MBINU ZA SIMBA ZAWATIBUA YANGA, PEDRO AJA KIVINGINE

KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Pedro Goncalves, ameonyesha dalili za kujipanga mapema kwa kuandaa mbinu mpya zitakazowasaidia kukabiliana na changamoto za wapinzani wao katika Ligi Kuu Tanzania Bara, kufuatia kile alichokiona kwenye mchezo uliopita wa Kariakoo Derby.

Pedro amesema kuwa katika dakika 30 za kipindi cha kwanza cha dabi dhidi ya Simba SC, walikutana na ushindani mkubwa baada ya wapinzani wao kubadili mfumo wa uchezaji. Mabadiliko hayo yaliwapa wakati mgumu na kuwalazimu kuchukua muda kurekebisha mipango yao kabla ya kuanza kuhimili presha.

Kocha huyo ameeleza kuwa Simba walionekana tofauti kabisa na alivyozoea kuwaona, hasa kwa namna walivyotumia mashambulizi ya kasi kupitia pembeni pamoja na mipira mirefu ya kushtukiza iliyolenga kuvunja safu yao ya ulinzi mapema.

“Namna walivyobadilisha mbinu zao na kuanza kwa mashambulizi ya kasi kutoka pembeni pamoja na mipira mirefu ya kushtukiza, ilikuwa changamoto kubwa kwetu. Hii tunatakiwa kuifanyia kazi kwa sababu kuna mechi nyingi zilizopo mbele yetu na wapinzani wanaweza kuja na mbinu tofauti. Tunapaswa kuwa tayari mapema,” amesema Pedro.

Ameongeza kuwa mchezo huo wa dabi ulikuwa funzo muhimu kwa kikosi chake, akisisitiza kuwa wanahitaji kujifunza haraka na kuboresha maeneo yaliyoonekana kuwa na udhaifu kabla ya kuingia kwenye michezo ijayo yenye ushindani mkubwa.

Kwa sasa, kikosi cha Yanga kimesafiri kuelekea Singida kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Singida Black Stars utakaopigwa Machi 5, 2026 katika Uwanja wa Airtel Stadium.

Yanga inauendea mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya sare ya bila kufungana kwenye dabi iliyopigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, huku Singida Black Stars wao wakiwa na morali baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union katika mchezo wao wa hivi karibuni.

Kwa mtazamo wa Pedro, mechi dhidi ya Singida ni mtihani mwingine wa kuthibitisha uimara wa kikosi chake na kurejesha makali katika mbio za kusaka alama tatu muhimu.

The post MBINU ZA SIMBA ZAWATIBUA YANGA, PEDRO AJA KIVINGINE appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/SOa4mBX
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post