YANGA YAPANGA KUIFUTA SIMANZI YA AFRIKA

MABINGWA watetezi wa Kombe la Shirikisho la CRDB, Yanga, leo wanashuka dimbani katika Uwanja wa KMC Complex kuvaana na Cosmopolitan kwenye mchezo wa hatua ya 64 bora utakaopigwa saa 1:00 usiku.

Yanga wanaingia katika pambano hilo wakiwa na morali ya juu kufuatia ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya JS Kabylie kwenye mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Licha ya ushindi huo kushindwa kuwavusha kwenda robo fainali, uliwarejeshea heshima na kuonyesha ubora wao mbele ya mashabiki.

Baada ya safari ya kimataifa kusimama, nguvu na akili za mabingwa hao wa Jangwani sasa zimeelekezwa kikamilifu kwenye mashindano ya ndani. Lengo ni moja tu kutetea ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB sambamba na kuendelea kupambana kwenye mbio za Ligi Kuu.

Kwa mtazamo wa vikosi, Yanga wanaonekana kuwa na faida kubwa kutokana na uzoefu wa wachezaji wao, ubora wa kikosi pamoja na benchi la ufundi lenye uzoefu.

Hata hivyo, historia ya michezo ya mtoano imeonyesha kuwa mechi za aina hii huwa na ushindani mkubwa, kwani timu ndogo huingia kwa ari ya ziada wakisaka matokeo ya kushtua.

Upande wa Cosmopolitan, mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu msimu wa 1967/68, wanakuja na hamasa yao wenyewe. Kwa sasa wanashika nafasi ya pili kwenye kundi lao la First League wakiwa na pointi 13 baada ya michezo saba, takwimu zinazoonyesha wazi kuwa si wapinzani wa kubeza.

Kwao, huu ni mchezo wa kihistoria na jukwaa la kujitangaza. Motisha ya kucheza dhidi ya mabingwa watetezi inaweza kuwapa nguvu ya ziada na kuingia uwanjani kwa tahadhari, nidhamu na presha ndogo.

Kwa Yanga, ushindi wa leo ni muhimu ili kuanza kwa hatua thabiti safari ya kutetea taji lao. Hata hivyo, wanapaswa kuwa makini na kuepuka kuingia uwanjani kwa dharau, kwani michezo ya mtoano mara nyingi hubeba matokeo yasiyotabirika.

The post YANGA YAPANGA KUIFUTA SIMANZI YA AFRIKA appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/U6yeIMZ
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post