LICHA ya ndoto ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuonekana kuyeyuka, uongozi wa Klabu ya Simba umewataka mashabiki wake kuendelea kuwa imara, kutokata tamaa na kuisapoti timu hiyo kwa hali na mali.
Simba imejikuta ikibaki mkiani mwa Kundi D ikiwa na pointi moja baada ya kucheza michezo minne, hali iliyotokana na sare ya mabao 2-2 dhidi ya Esperance de Tunis. Matokeo hayo yamepunguza rasmi matumaini ya kusonga mbele katika michuano hiyo mikubwa ya kimataifa.
Kupitia ukurasa wake rasmi mtandao ya kijamii, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amewaomba mashabiki wa klabu hiyo kutoruhusu matokeo ya msimu huu yawavunje moyo wala kuwaingiza katika unyonge.
Ahmed amesema kuwa kushindwa kufanya vizuri kimataifa msimu huu kunapaswa kuwa chachu ya kujipanga upya badala ya sababu ya kukata tamaa.
Ameeleza kuwa mafanikio makubwa huanza na changamoto, akisisitiza kuwa Simba imewahi kuipa heshima kubwa Tanzania na Afrika kwa ujumla.
“Wakati mwingine ili ufike juu ni lazima uanzie chini. Msimu huu tumeteleza, lakini tusiivunjie adabu timu yetu ambayo imetupa heshima kubwa Afrika,” ameandika Ahmed.
Ameongeza kuwa yapo makundi yanayotumia matokeo hayo kuchochea mgawanyiko kwa mashabiki na viongozi wa klabu, akiwataka Wanasimba kuwa makini na kuchagua nini cha kusikiliza na nini cha kuzungumza kwa maslahi ya klabu yao.
“Tuilinde nembo ya klabu yetu. Mnyama atarejea kwenye ufalme wake tena hivi punde,” ameongeza Meneja huyo.
Kwa sasa, Simba bado inasubiri kumaliza ratiba ya michezo miwili iliyobaki ya hatua ya makundi, ikianza na ugenini dhidi ya Petro de Luanda Februari 6, kabla ya kuikaribisha Stade Malien Februari 13 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
The post SIMBA MSIKATE TAMAA, UMOJA NDIO NJIA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/dv7CkZ5
via IFTTT
Post a Comment