SIMBA KUMALIZA RATIBA CAFCL, UONGOZI WATOA AHADI

MTENDAJI Mkuu wa Simba SC, Zubeda Sakuru, amesema kila mwisho ni mwanzo wa maandalizi mapya na kujipanga upya kwa mafanikio yajayo.

Amesema  safari ya timu hiyo katika mashindano ya kimataifa msimu huu imefikia tamati huku matarajio yao makubwa yakishindwa kufikiwa kama walivyopanga mwanzoni.

Simba leo inashuka dimbani kukamilisha ratiba kwa kucheza mchezo wa mwisho wa hatua ya mKundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Stade Malien utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam saa 1:00 usiku.

Ameeleza kuwa walipoanza msimu walikuwa na nguvu na ari kubwa, wakiamini wanaweza kufika mbali zaidi, lakini changamoto kadhaa zilijitokeza njiani na kulazimu kufanyika kwa mabadiliko mbalimbali ndani ya kikosi ili kurejesha ladha na utambulisho wa soka la Msimbazi.

Amesema mchezo wa leo ni wa mwisho kwa Simba katika jukwaa la kimataifa msimu huu,  kuwa licha ya kuwa ni “Last Dance” kwa kampeni hii, si mwisho wa safari ya klabu hiyo yenye historia kubwa nchini na barani Afrika.

Zubeda amewashukuru mashabiki, wapenzi na wanachama wa Simba kwa kuendelea kuiunga mkono klabu yao katika nyakati zote,  iwe za furaha au changamoto.

Amepongeza moyo wao wa kujitoa, kusafiri umbali mrefu, kuvumilia jua na mvua, pamoja na kuikosoa timu pale inapohitajika, akieleza kuwa yote hayo ni sehemu ya kulinda heshima na hadhi ya klabu.

“Vilabu bora hukumbwa na dhoruba, lakini mashabiki bora hubeba jahazi lisipinduke,” amesema, amesisitiza kuwa mshikamano ndio silaha kubwa ya mafanikio.

Ameongeza kwa kuwataka Wanasimba kuendelea kuishi falsafa ya klabu yao ya Simba, Nguvu Moja, na kuungana kwa mara nyingine kuisapoti timu katika mchezo wa leo utakaopigwa Uwanja wa Lupaso.

The post SIMBA KUMALIZA RATIBA CAFCL, UONGOZI WATOA AHADI appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/LcVlBPC
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post