OURA AOMBA MSHIKAMANO SIMBA, ONYO KALI

MSHAMBULIAJI wa Simba, Anicet Oura, ameomba ushirikiano mkubwa ndani ya kikosi cha timu hiyo ili waweze kuendelea kufanya vizuri na kuisaidia timu kupata matokeo chanya katika kila mechi wanayocheza msimu huu.

Nyota huyo ambaye alijiunga na Simba SC katika dirisha dogo la usajili, ujio wake ulikuwa ni mapendekezo ya benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu, Steve Barker, ambaye alihitaji kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji.

Tangu ajiunge na timu hiyo, Oura tayari ameonyesha mchango wake kwa kufunga mabao mawili katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo, Simba haikuwa na msimu mzuri kimataifa baada ya kushindwa kuvuka hatua ya makundi, licha ya kumaliza kwa ushindi katika mechi yao ya mwisho dhidi ya Stade Malien. Ushindi huo umeonekana kuwa faraja kwa kikosi hicho kuelekea majukumu ya ndani.

Oura amesema anafurahia kuaminiwa na kupewa nafasi ndani ya kikosi hicho kikubwa, amesisitiza kuwa yupo tayari kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha anaisaidia timu kupata alama muhimu katika kila mchezo, hususan katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Hatukuwa na msimu mzuri kimataifa, lakini ushindi tulioupata katika mechi ya mwisho ni muhimu kwetu. Umeturudishia morali na nguvu ya kupambana zaidi katika ligi ya nyumbani,” amesema mshambuliaji huyo.

Ameongeza kuwa ushirikiano uliopo ndani ya kikosi hicho ni mkubwa na unazidi kuimarika kadri siku zinavyosonga mbele,  wachezaji wapya wameanza kuzoea mfumo na kujenga uelewano mzuri na wale waliokuwepo awali, jambo linalompa matumaini makubwa ya kuona Simba ikirejea katika ubora wake na kufanya vizuri katika mechi zijazo.

The post OURA AOMBA MSHIKAMANO SIMBA, ONYO KALI appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/r0OGXhd
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post