MANGUNGU AVUNJA UKIMYA SIMBA, HATUJIUZULU

MWENYEKITI wa Klabu ya Simba na Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Murtaza Mangungu, amesema uongozi wa klabu hiyo unaendelea kutekeleza majukumu yake kama inavyoelekezwa na katiba, huku akisisitiza kuwa tathmini ya viongozi hufanyika pale muda unapofika.

Mangungu amesema kwa sasa wao kama viongozi wako kazini na hawajafikia hatua ya kujitathmini, akieleza kuwa itakapofika muda sahihi ndipo watakapokaa chini na kufanya tathmini ya kina kuhusu nafasi zao ndani ya uongozi wa klabu.

Kauli hiyo inakuja kufuatia baadhi ya Wanachama na Mashabiki wa Simba kuibua wito wa kumtaka Mwenyekiti huyo kujiuzulu, wakieleza kutoridhishwa na mwenendo wa timu katika mashindano ya kimataifa msimu huu.

Simba imekuwa na matokeo yasiyoridhisha msimu huu, ikiwemo kupoteza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, kutoka sare na Mtibwa Sugar, pamoja na kushindwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumzia presha na makelele kutoka kwa baadhi ya wanachama, Mangungu amesema bado anaendelea na majukumu yake ya kiuongozi bila kuyumbishwa, akisisitiza kuwa haogopi presha wala kelele zisizo na msingi.

“Uongozi ni wa muda na tathmini sahihi hufanywa wakati muafaka unapofika. Uongozi wa Simba si wa mtu mmoja, na baada ya muda wetu kufika tutakaa chini kujitathmini kama tunaweza kuendelea kugombea au kukaa pembeni na kuwaachia wengine,” amesema Mangungu.

Ameongeza kuwa kwa sasa anaendelea kuratibu mipango na mikakati ya maendeleo ya klabu hadi mwisho wa kipindi chao cha uongozi, huku akibainisha kuwa licha ya kuwepo kwa wachache wanaopinga, bado anaungwa mkono na idadi kubwa ya Wanachama na Mashabiki wa Simba.

“Wapo wengi wanaoniunga mkono, wananipa moyo wa kuendelea kuitumikia Simba na kunishauri mambo yanayopaswa kurekebishwa. Kwa sasa bado tupo kazini na tutaendelea kuwatumikia Wanasimba kwa bidii hadi pale itakapofika mwisho wa muda wetu au mabadiliko mengine kufanyika kwa mujibu wa taratibu za klabu,” amesema.

The post MANGUNGU AVUNJA UKIMYA SIMBA, HATUJIUZULU appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/SB3LwX2
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post