BEKI wa kushoto wa Singida Black Stars, Mghana Ibrahim Imoro, amehusika katika mabao matatu ya Ligi Kuu Bara msimu huu, huku kati ya hayo mawili nyota huyo ameyatoa dhidi ya kikosi cha Fountain Gate, tena akizichezea timu mbili tofauti.
Nyota huyo alitoa asisti yake ya kwanza msimu huu ya bao la mshambuliaji, Andrew Simchimba dakika ya 16, katika ushindi wa Mtibwa Sugar wa mabao 2-0, dhidi ya Fountain Gate, Septemba 28, 2025, huku Lamela Maneno akijifunga mwenyewe la pili.
Asisti ya pili kwa Imoro aliitoa pia katika ushindi wa Mtibwa Sugar aliyojiunga nayo mwanzoni mwa msimu huu kwa mkopo, akitokea Singida Black Stars, wakati kikosi hicho kilipoifunga TRA United mabao 2-1, mechi ikipigwa, Novemba 29, 2025.
Baada ya kuitumikia Mtibwa, nyota huyo akarejea tena Singida katika dirisha dogo la Januari 2026, ambapo alichangia pia bao la ushindi wa timu hiyo wa 1-0, dhidi ya Fountain Gate, Februari 11, 2026, lililofungwa na Mkongomani Linda Mtange.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam, Imoro aliingia katika dk57, akichukua nafasi ya Rahim Shomary, ambapo katika dakika ya 64, alipiga krosi safi iliyounganishwa vizuri na Mtange. Imoro alijiunga na timu hiyo Julai 1, 2024, akitokea Al-Hilal Omdurman ya Sudan.
Awali, alikuwa anawindwa na matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC, ingawa dili hilo lilifeli na kutimkia Mtibwa Sugar aliyoichezea mwanzo wa msimu huu.
Kiwango kizuri alichokionyesha akiwa na Mtibwa Sugar tangu msimu umeanza nyota huyo aliyewahi kuchezea Bolga All Stars, Karela United na Asante Kotoko za Ghana, kikawafanya mabosi wa Singida kumrejesha katika dirisha dogo la Januari 2026.
The post KUNA HII YA IBRAHIM IMORO SINGIDA BLACK STARS appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/oBnyj3m
via IFTTT
Post a Comment