MSHAMBULIAJI wa Coastal Union, Shiza Kichuya amesema kasi aliyoanza nayo akiwa na kikosi hicho katika kufumania nyavu, inampa nguvu ya kupiga hesabu kali zaidi ili kufunga mengi kuliko ilivyokuwa msimu uliopita akiwa na JKT Tanzania.
Nyota huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, Simba na Namungo aliyewahi kucheza soka la kulipwa Misri, aliliambia Mwanaspoti, anatamani msimu huu afunge mabao zaidi ya manne aliyomaliza nayo msimu uliopita akiwa na JKT Tanzania, japo amekiri ushindani katika Ligi Kuu msimu huu ni mkubwa.
Kichuya aliyejiunga na Coastal katika usajili wa dirisha dogo, akiwa na timu hiyo ameishafunga mabao matatu, jambo ambalo anaamini kuna uwezekano mkubwa Ligi Kuu inayoendelea akamaliza na mabao mengi.
“Siwezi kusema nitamaliza na mabao mangapi, lakini natamani kuvuka idadi ya mabao manne niliyofunga msimu uliopita, ushindani ni mkali na ligi ni ngumu, lakini kazi ya wachezaji ni kupambania timu,” amesema Kichuya na kuongeza;
“Ukiachana na malengo yangu binafsi, kipaumbele cha kila mchezaji ni kuhakikisha timu ya Coastal inamaliza ikiwa katika nafasi za juu, mafanikio ya timu ndiyo mafanikio ya mchezaji.
“Furaha ya mchezaji msimu unapomalizika timu iwe imefikia malengo yake, nje na hapo ni maumivu makali, wenzetu wanakwenda kupumzika mnakuwa mnapambana kucheza mtoano, ndiyo maana tunajituma na kupambana ili kulitimiza hilo.”
Akiwa na Simba aliyojiunga nayo 2016 alipata umaarufu mkubwa kutokana na kuifunga Yanga katika mechi za dabi ikiwamo bao la kona ya moja kwa moja Oktoba Mosi, 2016.
Mpira wa kona aliyoichonga ulimshinda aliyekuwa kipa wa Wanajangwani, Ally Mustapha ‘Barthez’, mechi hiyo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Msimu mzuri zaidi kwake ni ule wa 2016-2017 akiwa Simba alipofunga mabao 12 akilingana na Mbaraka Yusuf aliyekuwa Kagera Sugar na Obrey Chirwa alipokuwa Yanga, waliokuwa nyuma ya vinara wa msimu, Simon Msuva na Abdulrahman Mussa waliokuwa Yanga na Ruvu Shiooting waliomaliza na mabao 14 kila mmoja.
The post KICHUYA APIGA HESABU KALI COASTAL UNION appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/WtrZwn3
via IFTTT
Post a Comment