KIBU AAGA RASMI SIMBA, RASMI ATIMKIA LIBYA

MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Kibu Denis, ameweka wazi kile alichokiita dhamira ya wachezaji wa kikosi hicho kambini, akiwataka waendelee kupambana kufikia malengo waliyojiwekea msimu huu, ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kibu ameaga rasmi wachezaji wenzake baada ya kulitumikia klabu hiyo kwa mafanikio kwa kipindi cha miaka minne na nusu, akifunga ukurasa wa safari yake Msimbazi na kuanza changamoto mpya katika klabu ya Al Nasr ya Libya.

Akizungumza wakati wa kuaga, nyota huyo amesema atafurahi kuona Simba ikitimiza malengo yake ya msimu huu na kuendelea kuwapa furaha Wanasimba, amesisitiza umuhimu wa mshikamano na kusimama imara katika mipango waliyojiwekea.

“Kwa miaka minne na nusu nimefanya kazi Simba. Sasa nimepata sehemu nyingine ya kwenda kuanza ukurasa mpya na kutengeneza familia,Nawashukuru wachezaji wenzangu kwa sapoti waliyonipa kama rafiki, familia na ndugu. Pia nawashukuru benchi la ufundi,” amesema  Kibu.

Aliongeza kuwa kikubwa kwa sasa ni wachezaji kusimama katika mipango yao ya kuhakikisha Simba inafikia malengo waliyojiwekea, hususan kupigania ubingwa wa Ligi Kuu.

Mbali na hilo, Kibu amewashukuru  wachezaji wenzake kwa ushirikiano na upendo waliomuonesha, akiwataja kama familia yake ya pili ndani na nje ya uwanja.

Uhamisho wake kwenda Al Nasr Benghazi unaongeza idadi ya nyota waliowahi kuichezea Simba ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na aliyekuwa kocha wa Wekundu wa Msimbazi, Fadlu Davids.

Wengine waliotoka Simba na kujiunga na Al Nasr ni Fabrice Ngoma na Steven Mukwala. Kibu anaondoka akiwa miongoni mwa wachezaji tegemeo katika safu ya ushambuliaji, akitoa mchango mkubwa katika mashindano ya ndani na kimataifa.

Uwezo wake wa kucheza zaidi ya nafasi moja katika eneo la ushambuliaji ulimfanya kuwa silaha muhimu kwa makocha tofauti waliowahi kuinoa Simba katika kipindi chake chote cha mafanikio klabuni hapo.

The post KIBU AAGA RASMI SIMBA, RASMI ATIMKIA LIBYA appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/DPrCANJ
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post