KAULI ya “mwenda pole ndiye mla nyama” inaendelea kuidhihirisha vyema falsafa ya uongozi wa Klabu ya Simba katika mikakati yao ya usajili wa dirisha dogo, wakilenga kuimarisha kikosi kwa utulivu na umakini mkubwa.
Wakati baadhi ya timu tayari zimeanza kutambulisha silaha zao mpya hadharani, Simba wao wamechagua kufanya kazi kimya kimya, wakipima kila hatua kwa maslahi ya muda mrefu ya klabu.
Taarifa zinaeleza kuwa uongozi wa Simba umeingia kwenye mazungumzo na aliyekuwa nyota wa Singida Black Stars, Antony Tra Bi Tra, kwa lengo la kumsajili kama mchezaji huru.
Sambamba na hilo, kiungo wa Kenya Police FC, Charles Ouma, kwa sasa yupo nchini akifanya mazoezi na kikosi cha Simba, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kumtathmini kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.
Chanzo cha karibu na klabu kinasema Antony Tra Bi Tra ni miongoni mwa viungo bora waliowahi kuichezea Singida Black Stars, huku Simba wakimfuatilia kwa muda mrefu hata kabla ya kujiunga na klabu hiyo.
Uzoefu wake na ubora aliouonesha umemfanya kuwa mmoja wa wachezaji wanaotazamwa kwa jicho la kipekee na wekundu wa Msimbazi.
“Uvunjwaji wa mkataba wake kwa makubaliano ya pande zote unawapa Simba nafasi ya dhahabu kumnasa bila gharama ya uhamisho,” kimesema chanzo hicho, kikibainisha kuwa hilo linaifanya dili hiyo kuwa ya kimkakati na yenye faida kubwa kwa klabu.
Kwa upande wa Ouma, imeelezwa kuwa atakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kitakachoshiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayoendelea visiwani Zanzibar. Kocha Mkuu Steve Barker atapata nafasi ya kumtazama kwa karibu katika mazingira ya ushindani kabla ya kutoa mapendekezo ya mwisho juu ya usajili wake.
“Kocha atakuwa na jukumu la kumtazama kiungo huyo kutoka Kenya Police, na endapo ataridhishwa na kiwango chake, basi Simba wanaweza kumsajili katika dirisha hili dogo,” kiliongeza chanzo hicho.
Akizungumza kuhusu suala la usajili, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, amesema kuna uwezekano wa klabu kuongeza wachezaji zaidi ya hao wawili, ingawa ni mapema kuyazungumzia majina mengine.
Ameeleza kuwa dirisha la usajili ni kipindi cha kuimarisha kikosi, hasa wakati huu ambao baadhi ya wachezaji wapo kwenye majukumu ya timu za Taifa.
“Kwa sasa tupo kwenye mashindano ya Mapinduzi, tumeongeza baadhi ya wachezaji kusaidia kikosi kwa sababu wengine wapo kwenye timu za Taifa. Pia tumewachukua vijana, tukizingatia ligi inaendelea, hivyo tunatumia wachezaji wanaokuja kuangaliwa. Ikifika muda sahihi, majina ya waliosajiliwa yatatangazwa rasmi,” amesema Rweyemamu.
The post SIMBA MWENDA POLE NDIE MLA NYAMA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/CVIpQTK
via IFTTT
Post a Comment