MENEJA Mkuu wa Singida Black Stars, Othmen Najjar, ameonekana kulivuruga benchi la ufundi la Yanga baada ya kuchukua uamuzi wa kumrejesha kiungo Marouf Tchakei ndani ya kikosi cha Singida Black Stars, maarufu kama Walima Alizeti.
Marouf, ambaye alikuwa amejiunga na Yanga kwa makubaliano ya mkopo wa miezi sita, aliitumikia klabu hiyo katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi, akionesha kiwango kilichowavutia mashabiki na benchi la ufundi la Wananchi.
Hata hivyo, ujio wa Meneja Najjar ndani ya kikosi cha Singida Black Stars umebadilisha mwelekeo wa makubaliano hayo. Baada ya kumshuhudia Marouf akicheza akiwa na jezi za Yanga, Najjar aliutaka uongozi wa klabu hiyo kuhakikisha kiungo huyo anarejea kwa waajiri wake halali.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, amesema meneja wao amesitisha rasmi makubaliano yaliyokuwapo kati ya Singida Black Stars na Yanga kuhusu mkopo wa Marouf.
Massanza ameeleza kuwa awali kulikuwa na makubaliano ya kuwaruhusu nyota wao wawili, Marouf Tchakei na Mohamed Damaro, kwenda kwa mkopo Yanga, jambo lililothibitishwa na wachezaji hao kuonekana wakizivaa jezi za klabu hiyo ya Jangwani.
“Hata hivyo, baada ya ujio wa Meneja wetu na kubaini mapungufu ndani ya kikosi, aliamua kuzuia dili la Marouf kuendelea kuitumikia Yanga na badala yake kurejea kikosini kuisaidia Singida Black Stars,” amesema Massanza
The post NAJJAR AIVURUGA YANGA VIBAYA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/LhAal59
via IFTTT
Post a Comment