MBWA MWITU AINGIA RASMI NDANI YA YANGA

ALIYEKUWA mshambuliaji wa Radomiak Radom ya Poland, Laurindo Dilson Maria Aurelio maarufu kwa jina la Mbwa Mwitu (Depu), ametambulishwa rasmi kuwa mchezaji wa klabu ya Yanga SC, hatua inayoongeza nguvu mpya katika kikosi cha mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Depu amesajiliwa katika dirisha dogo la usajili kwa lengo la kuimarisha safu ya ushambuliaji ya Yanga, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa klabu hiyo kuongeza ushindani na ufanisi kuelekea nusu ya pili ya msimu. Ujio wake unaashiria dhamira ya dhati ya Yanga kuendelea kuwa imara ndani na nje ya nchi.

Mshambuliaji huyo raia wa Angola anakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na Yanga katika dirisha hili dogo, akijiunga na Emmanuel Mwanengo, Mohammed Damaro pamoja na Allan Okello ambaye alitambulishwa rasmi siku chache zilizopita.

Ujio wa Depu pia unaambatana na kurejea kufanya kazi chini ya kocha wake wa zamani, Pedro Goncalves. Hali hiyo inaaminika itamsaidia mchezaji huyo kuzoea kwa haraka falsafa ya timu, mfumo wa uchezaji pamoja na mahitaji ya benchi la ufundi.

Yanga imeendelea kuonesha nia thabiti ya kuboresha kikosi chake ili kudumisha ushindani katika mashindano ya ndani na yale ya kimataifa. Usajili wa Depu unatarajiwa kuongeza ushindani mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji na kutoa chaguo zaidi kwa benchi la ufundi.

Kwa uwezo wake mzuri wa kufumania nyavu akiwa anacheza nafasi ya namba tisa, Laurindo ‘Depu’ anatarajiwa kuwa silaha muhimu kwa Yanga, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona mchango wake ndani ya uwanja.

The post MBWA MWITU AINGIA RASMI NDANI YA YANGA appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/QErBLIa
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post