BAADA ya kusubiri kwa miaka minne, klabu ya Yanga SC imerejea kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2026, baada ya kuibuka na ushindi wa penalti 5-4 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja wa Gombani, Pemba.
Mchezo huo wa fainali ulikuwa na ushindani mkubwa kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho, huku timu zote zikionesha nidhamu ya hali ya juu ya kiufundi.
Dakika 90 za kawaida zilimalizika kwa sare ya bila kufungana, hali iliyolazimu kuongezwa kwa dakika 30 za muda wa ziada, lakini bado hakuna timu iliyoweza kutikisa nyavu za mpinzani wake.
Katika kipindi cha kwanza cha mchezo, Azam FC na Yanga zilishambuliana kwa zamu, kila timu ikitafuta bao la mapema, lakini umakini wa walinzi na makipa ulifanya kipindi hicho kumalizika kwa sare ya 0-0.
Hali hiyo iliendelea hadi kipindi cha pili na muda wa ziada, ambapo nafasi chache zilizopatikana zilishindwa kutumika ipasavyo.
Yanga walipata nafasi ya wazi ya kufunga kupitia mkwaju wa penalti ndani ya dakika za kawaida baada ya beki wa Azam FC kucheza mpira wa mkono, hata hivyo Pacome Zouzoua alikosa penalti hiyo, na kuifanya timu yake kuendelea kusubiri ushindi hadi hatua ya mikwaju ya penalti.
Katika hatua ya penalti, Yanga walionyesha utulivu na umakini mkubwa, huku mikwaju yao ikifungwa na Emmanuel Mwanengo, Prince Dube, Pacome Zouzoua, Mudathir Yahya pamoja na Bakari Mwamnyeto aliyepiga penalti ya mwisho na kuipa Yanga ushindi wa 5-4 dhidi ya Azam FC.
Shujaa wa Yanga, Mwamnyeto, alikuwa na safari ndefu kutoka Morocco hadi Pemba, baada ya kujiunga na kikosi hicho jana akitokea katika majukumu ya timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) iliyokuwa ikishiriki fainali za AFCON nchini Morocco, na mchango wake ulihitimishwa kwa penalti ya ushindi.
Kwa ushindi huo, Yanga wametawazwa mabingwa wa Kombe la Mapinduzi kwa mara ya kwanza tangu walipotwaa taji hilo mwaka 2021, ushindi unaowapa morali kubwa kuelekea michuano ijayo ya ndani na kimataifa.
The post KUTOKA MOROCCO HADI PEMBA KUIPA YANGA UBINGWA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/aGzZHul
via IFTTT
Post a Comment