LICHA ya kuwa walitokea Singida Black Stars, nyota wawili wa Yanga, Mohammed Damaro na Marouf Tchakei, wanatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka dimbani kuikabili timu hiyo katika mchezo wa nusu fainali ya pili ya Kombe la Mapinduzi.
Yanga inashuka katika dimba la New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, kesho kuwakabili Singida Black Stars katika pambano linalotarajiwa kuwa gumu na lenye ushindani mkubwa, huku kila timu ikisaka nafasi ya kutinga fainali.
Damaro na Marouf wamejiunga na Yanga kwa mkataba wa mkopo wa miezi sita wakitokea Singida Black Stars, mkataba ambao utadumu hadi mwishoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Uamuzi wa kuwaruhusu nyota hao kucheza dhidi ya waajiri wao wa zamani umeondoa sintofahamu iliyokuwepo miongoni mwa mashabiki wa soka, hasa ikizingatiwa umuhimu wa mchezo huo katika hatua ya mtoano.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema Damaro na Marouf ni wachezaji halali wa klabu hiyo kwa sasa na watakuwa sehemu ya kikosi cha mechi hiyo muhimu.
“Hao ni wachezaji wa Yanga kwa sasa, watakuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka dimbani kesho. Suala la kuanza au kuanzia benchi ni maamuzi ya benchi la ufundi chini ya kocha wetu Pedro Goncalves,” amesema Kamwe.
Mshindi atakayepatikana atatinga fainali ya Kombe la Mapinduzi na kukutana na mshindi wa nusu fainali ya kwanza kati ya Simba SC na Azam FC, mchezo unaochezwa leo saa 2:15 usiku katika dimba hilo hilo la New Amaan Complex.
The post DAMARO, MAROUF KUIKABILI SINGIDA NUSU FAINALI appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/UitLaSw
via IFTTT
Post a Comment