BAJEBER BADO ANAJITAFUTA

WAKATI mashabiki wa Simba  wakizidi kufurahishwa na mchango wa mshambuliaji wao, Mohammed Bajeber, nyota huyo ameweka wazi kuwa bado hajafikia kiwango chake cha juu cha ufiti.

Amesema  kuwa kile anachokionesha uwanjani ni sehemu ya safari ya kurejea kwenye ubora wake kamili.

Bajeber amesema licha ya kufanikiwa kuipatia Simba mabao mawili muhimu, moja katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na lingine kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, mechi hizo zimekuwa sehemu ya mchakato wake wa kurejesha makali baada ya kipindi kirefu cha majeraha.

Mshambuliaji huyo alijiunga na Simba SC katika dirisha kubwa la usajili akitokea nchini Kenya, bado hajarejea kikamilifu baada ya majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda.

Hata hivyo, baada ya kupona ameanza kupewa nafasi ya kucheza, akianza dhidi ya Mbeya City na kufunga bao lake la kwanza tangu atue ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.

Amesema mapumziko yaliyokuwepo kabla ya kurejea kambini yalikuwa na mchango mkubwa katika kumsaidia kujiandaa vyema, kwani aliyatumia kufanya mazoezi binafsi yaliyolenga kuongeza ufiti na kurejesha nguvu ya mwili.

Bajeber ameongeza kuwa michuano ya Kombe la Mapinduzi kwake ni fursa muhimu ya kuendelea kujipima na kujinoa zaidi, akitambua kuwa bado ana safari ndefu ya kufikia kiwango bora kinachotarajiwa na mashabiki pamoja na benchi la ufundi.

“Nilitumia mapumziko kufanya mazoezi yangu binafsi ili kujiweka fiti zaidi. Ingawa tayari nimerudi uwanjani, nimecheza mechi mbili na kufunga mabao ikiwemo dhidi ya Mbeya City na kwenye Kombe la Mapinduzi, bado natafuta ufiti wangu kamili,” amesema Bajeber.

mshambuliaji huyo amesema suala la kufikia ufiti wa asilimia 100 linahitaji subira na kumwachia Mungu, huku akibainisha kuwa licha ya matokeo mazuri yanayoonekana, kikosi bado kinaendelea kujijenga hasa ikizingatiwa kuwa benchi la ufundi ni jipya na bado linaendelea kutengeneza mwelekeo wa timu.

The post BAJEBER BADO ANAJITAFUTA appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/2yq3b98
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post