MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema kuwa hali ya mambo ilivyokuwa wiki moja iliyopita ingeweza kumfanya Mwanasimba yeyote kukata tamaa, lakini kwa Simba ya sasa hilo halipaswi kuwa chaguo.
Ahmed amesema kuwa pamoja na changamoto zinazolikabili timu, Mwanasimba anaruhusiwa kukata chochote, hata roho, lakini siyo kukata tamaa.
Ameeleza kuwa ndani ya kikosi bado kuna imani, uwezo na morali kubwa ya kupambana hadi dakika ya mwisho kwa ajili ya kulinda heshima ya klabu hiyo.
Amefafanua kuwa Simba bado ina nafasi kubwa ya kufanya maajabu katika Ligi ya Mabingwa Afrika, huku lengo kuu likiwa ni kukusanya alama tisa katika michezo mitatu iliyosalia ili kufikia malengo waliojiwekea msimu huu.
Kwa mujibu wa Ahmed, Simba inapaswa kushinda michezo yote mitatu iliyosalia, ikianza na Esperance Sportive de Tunis katika mchezo utakaochezwa Jumapili Februari 1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Baada ya hapo, Simba itasafiri kwenda Angola kuivaa Petro de Luanda kabla ya kurejea nyumbani kuhitimisha kampeni dhidi ya Stade Malien, ikiwa ni jitihada za kupanda kutoka nafasi za chini za msimamo na kuishtua Afrika.
“Nipo hapa kuwathibitishia Wanasimba kwamba Mnyama bado ana matumaini na uwezo mkubwa wa kuchukua alama tisa katika mechi hizi tatu. Kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu na ubora wa wachezaji wetu, hili linawezekana,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa bado kuna wachezaji muhimu ambao hawajapata nafasi ya kucheza, akimtaja kiungo mshambuliaji Inno Loemba kutoka Congo Brazzaville, hali ambayo imeongeza matumaini na kuimarisha ujasiri ndani ya kikosi hicho kuelekea michezo ijayo.
The post AHMED, MWANASIMBA KATA CHOCHOTE USIKATE TAMAA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/GsXIh3Z
via IFTTT
Post a Comment