KLABU ya Yanga imeweka wazi mpango wake wa kufanya maboresho kwenye kikosi chake baada ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili la Ligi Kuu Tanzania Bara, ikieleza kuwa itafanya usajili wa wachezaji wasiopungua watatu.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa inatokana na ripoti ya kocha mkuu wa timu hiyo, Pedro Goncalves, ambayo imeainisha maeneo yanayohitaji kuimarishwa ili kuongeza ushindani na ufanisi wa kikosi kuelekea nusu ya pili ya msimu.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema ripoti ya kocha Pedro tayari imeanza kufanyiwa kazi kwa asilimia 85 na mambo yanaendelea vizuri, huku uongozi ukihakikisha mahitaji yote ya kikosi yanazingatiwa kabla ya kukamilisha usajili.
Kamwe ameeleza kuwa pamoja na kutotaja majina ya wachezaji wanaozungumziwa, uongozi wa klabu hiyo unaendelea na mazungumzo na baadhi ya nyota, akiwemo mshambuliaji Laurindo Dilson Maria Aurelio maarufu kama ‘Dupe’.
Ameongeza kuwa dirisha dogo la usajili halilengi kufanya mabadiliko makubwa bali kuboresha kikosi kwa kuongeza nguvu katika maeneo yenye upungufu kulingana na tathmini ya benchi la ufundi.
Kwa mujibu wa Kamwe, Yanga inatafuta wachezaji watakaokuja kuongeza ushindani wa ndani na kutoa changamoto kwa wachezaji waliopo tayari, jambo litakalosaidia kuinua kiwango cha timu kwa ujumla.
“Tutasajili wachezaji wasiopungua watatu kulingana na ripoti ilivyoeleza. Hili si dirisha la kuhabatisha, tunasajili wachezaji watakaosaidia kufikia malengo ya klabu na kuongeza ushindani ndani ya kikosi,” amesema Kamwe.
The post YANGA WAIBUKA NA HAYA WAANIKA USAJILI WAO appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/Cz35pxq
via IFTTT
Post a Comment