KLABU ya Yanga imeanza rasmi mazungumzo ya kumsajili kiungo mshambuliaji wa Vipers SC ya Uganda, Allan Okello katika harakati zake za kuimarisha kikosi hicho kuelekea dirisha dogo la usajili la mwezi Januari.
Taarifa zinadai kuwa uongozi wa Yanga umeingia kwenye mazungumzo ya moja kwa moja na mchezaji huyo pamoja na wawakilishi wake, wakilenga kumalizana mapema ili kumleta nchini.
Okello, ambaye ni mchezaji muhimu ndani ya kikosi cha Vipers na timu ya taifa ya Uganda, ameendelea kuonyesha kiwango cha juu katika michuano mbalimbali, hali iliyomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaofuatiliwa kwa karibu na klabu kadhaa za Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa vyanzo vya karibu na klabu hiyo, Rais wa Yanga, Hersi Said amekuwa mstari wa mbele katika mazungumzo hayo akionesha nia ya dhati ya kuhakikisha usajili huo unakamilika kwa mafanikio, ili kuongeza ubora katika eneo la kiungo.
Ujio wa Okello endapo utakamilika unatarajiwa kuongeza ushindani mkubwa ndani ya kikosi cha Yanga, hasa katika nafasi za ushambuliaji wa kati, huku kocha akipata chaguo zaidi kuelekea mechi ngumu za ndani na kimataifa.
Hata hivyo, bado hakuna tamko rasmi kutoka kwa Yanga wala Vipers SC kuhusu hatua ya mwisho ya mazungumzo hayo, ingawa muda wowote kuanzia sasa chochote kinaweza kutokea kutokana na kasi ya majadiliano.
Mashabiki wa Yanga wanaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya dili hilo, wakisubiri kuona kama Okello atakuwa nyongeza mpya katika kikosi chao Januari hii, katika msimu unaohitaji ushindani mkubwa na ubora wa hali ya juu.
The post YANGA WAANZA MAZUNGUMZO NA ALLAN OKELLO appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/3FpSwaC
via IFTTT
Post a Comment