WAARABU NOMA…WATENGA BIL 15 KUMBEBA FEI TOTO AZAM ….DILI LENYEWE LIKO HIVI….

BAADA ya kutulia kwa siku kadhaa, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amerudi tena katika kutengeneza vichwa vya habari. Tena safari hii kwa kishindo kizito.

Kiungo mshambuliaji huyo maarufu pia kama Zanzibar Finest, alitawala vyombo vya habari kwa takribani miaka mitatu mfululizo, tangu alipojiunga na Azam FC mwaka 2023 akitokea Yanga.

Amekuwa akihusishwa na kuhamia klabu mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Kwa wanaokumbuka kipindi cha dirisha kubwa la usajili alihusishwa na Simba, Yanga, Kaizer Chiefs Afrika Kusini, lakini kwa bahati Agosti klabu inayommiliki ilitangaza kuwa ameongeza mkataba kuendelea kusalia Azam FC.

Lakini hivi karibuni akarudi tena kugonga vichwa vya habari kwa tetesi za kuhitajika na klabu ya Al Ahli Tripoli ya Libya. Ukurasa huu unaweza kuthibitisha taarifa hiyo na kukuletea undani wake kutoka vyanzo sahihi kabisa, ikiwamo kiwango cha Sh4.5 Bbilioni zilizowekwa mezani kumbeba!

ILIKOANZIA

Ni kweli kwamba Al Tripoli inahitaji huduma ya Fei Toto kwa sababu kuu mbili; kimpira na kisiasa.

KIMPIRA

Al Ahli Tripoli inayoshiriki Ligi Kuu ya Libya ina shida na namba kumi na katika upembuzi wao yakinifu wamebaini kwamba Fei Toto ni mtu sahihi kwao.

Wanaamini fika kwamba uwezo wake utaisaidia timu yao kufikia malengo.

KISIASA

Wanataka kumpata Fei Toto ili kushinda ile haki ya kujidai mtaani, yaani bragging rights.

Mashabiki wa Al Ahli Tripoli wamesisimuliwa sana na tetesi za klabu yao kumhitaji Fei na viongozi wanataka kupata heshima ya kisiasa kupitia usajili huo. Lakini zaidi ya hapo ni kuwakoga watani wao, Asswehly SC.

Timu hiyo ilivumishwa kumhitaji Feisal Salum kiasi ikasemekana walishaliweka jina lake hadi kwenye fomu za usajili…mwisho wa siku wakamkosa.

Sasa Al Ahli wakimpata, wanataka kuwakoga wapinzani wao…bragging rights!

ILIVYOKUJA KUWA

Al Ahli Tripoli kupitia kwa mawakala wao, wakamtafuta binafsi kiongozi mmoja wa Azam FC na kuelezea nia yao.

Akawajibu kwamba watume ofa ili klabu iipitie na kuona nini kitatokea.

Wakala akatuma ofa hiyo kupitia email yake binafsi…kwa huyo kiongozi na kwa mchezaji mwenyewe.

Hapa wakala alifanya kosa kubwa sana la kiufundi, kumtumia mchezaji ofa ambayo wameituma klabuni.

Kwanza sio sahihi na kilichowakera zaidi Azam FC ni kwamba wanahisi, ile iliyotumwa kwa mchezaji ndio iliyokuja kusambaa mitandaoni.

Ukweli ni kwamba ile ofa ni yenyewe kabisa…ila haikutumwa kutoka klabu kwenda klabu bali kutoka kwa wakala kwenda kwa kiongozi binafsi.

Yule kiongozi akamjibu yule wakala kwamba alichokifanya ni kitu cha hovyo na yeye binafsi hataki kuendelea kuongea nao.

Akamwambia kwamba kama klabu ina nia thabiti kumhitaji Fei, basi itume ofa kupitia anwani zao rasmi na waielekeze moja kwa moja katika anwani rasmi za Azam FC.

ILIVYO SASA

Wakala akafikisha ujumbe kwa Al Ahli Tripoli ambao bila ajizi wakatuma ofa yao moja kwa moja kwenye anwani za Azam FC. Hivi sasa Azam wanafanya tathmini yao ya kiufundi kuona kama waikubali au waikatae. Ofa yenyewe ni ya takribani Shilingi za Tanzania bilioni nne na nusu (Sh4.5 bilioni), sio ndogo hata kidogo.

Na mchezaji mwenyewe endapo atakubali, atapewa mkataba wa miaka minne wenye thamani ya jumla ya zaidi ya Shilingi za Tanzania bilioni 10. Hii ni thamani ya jumla, kwa maana ya pesa zake za kusainia mkataba na mshahara atakaolipwa katika wakati wake wote klabuni hapo…pamoja na motisha nyingine kama bonasi.

MSIMAMO WA MCHEZAJI

Al Ahli Tripoli wanamhitaji sana Fei Toto na walianza kwa kumshawishi wampe pesa avunje mkataba wake kama alivyofanya wakati anatoka Yanga.

Lakini yeye hataki kufanya hivyo, akiamini hatokuwa amewatendea haki Azam FC ambao wamempa heshima kubwa.

Ndio hapo wakaja na ofa kwa klabu. Feisal yuko tayari kwenda kucheza Libya, akiamini anastahili kutoka nje ya Tanzania…na anazihitaji pesa walizomwekea mezani.

Kama mambo yakienda vizuri, Fei Toto anaweza kuondoka dirisha dogo kwenda Libya na kumfanya kuwa mchezaji ghali zaidi kutoka Ligi ya Tanzania.

The post WAARABU NOMA…WATENGA BIL 15 KUMBEBA FEI TOTO AZAM ….DILI LENYEWE LIKO HIVI…. appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/pK5So8O
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post