IMEELEZWA kuwa klabu ya Yanga imekamilisha rasmi usajili wa mshambuliaji wa TRA United, Emmanuel Mwanengo maarufu kama ‘Mengo’, katika dirisha dogo la usajili linaloendelea.
Mengo amejiunga na Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kumalizika kwa mkataba wake na waajiri wake wa zamani TRA United, ambayo awali ilijulikana kama Tabora United.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo ya Jangwani, uongozi wa Yanga umefanikiwa kumshawishi nyota huyo kwa kumpa mkataba wa miaka miwili, utakaomuweka klabuni hapo hadi mwaka 2028.
Uongozi wa Yanga unaamini usajili wa Mengo utaongeza ushindani mkubwa katika safu ya ushambuliaji, hususan ikizingatiwa ratiba ngumu ya mashindano ya ndani na kimataifa yanayoikabili timu hiyo.
Mwanengo ana uwezo wa kucheza katika nafasi mbalimbali za ushambuliaji, ikiwemo winga wa kushoto, winga wa kulia, kiungo mshambuliaji na hata mshambuliaji wa kati, jambo linalompa kocha chaguo pana la kiufundi.
Usajili wa mshambuliaji huyo ni sehemu ya mapendekezo ya benchi la ufundi linaloongozwa na kocha mkuu Pedro Goncalves, ambaye amekuwa akisisitiza kuongezwa kwa wachezaji wazawa wenye uwezo wa kuleta tofauti.
Kupitia usajili huo, Yanga inaendelea kuonyesha dhamira yake ya kulinda taji la ligi pamoja na kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona mchango wa Mengo ndani ya kikosi hicho chenye ushindani mkubwa.
The post STRAIKA AONGEZWA KIKOSI CHA MABINGWA YANGA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/E0ykhZq
via IFTTT
Post a Comment