SIMBA WAFICHUA MIPANGO YA DIRISHA DOGO

UONGOZI wa Simba umeweka wazi mipango yao kuelekea dirisha dogo la usajili, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amethibitisha kuwa tayari kocha Selemani Matola amekabidhi ripoti kamili ya maeneo yanayohitaji kuongezewa nguvu.

Dirisha dogo linatarajiwa kufunguliwa Desemba 16 na kufungwa Januari 15, kipindi ambacho timu zote za Ligi Kuu na Championship zitapata nafasi ya kufanya maboresho katika vikosi vyao.

Kwa Simba, maandalizi hayo yameanza mapema ili kuhakikisha wanapata wachezaji sahihi kulingana na mahitaji ya benchi la ufundi.

Ahmed amesema ripoti ya kocha imebainisha mapungufu yaliyopo ndani ya kikosi na maeneo yanayohitaji kuongezewa nguvu, japokuwa amesisitiza kuwa hakutakuwa na mabadiliko makubwa kutokana na ukweli kwamba timu haijatumika sana msimu huu.

Simba imecheza mechi tano za ligi na mbili za kimataifa, hivyo bado wachezaji hawajapata nafasi ya kuonyesha ubora wao kikamilifu.

“Tunaenda kufanya mabadiliko machache, lakini yenye tija kulingana na mahitaji halisi ya kikosi. Tunachofanya sasa ni kutekeleza kile ambacho ripoti ya mwalimu imeelekeza,” alisema Ahmed.

Kuhusu taarifa zinazowahusisha Mzamiru Yassin na Awesu Awesu kutolewa kwa mkopo kwenda Mbeya City, Ahmed amekanusha vikali akisema hakuna maombi yoyote kutoka kwa klabu hiyo, wala Simba haijapokea taarifa za aina hiyo.

Simba imeonyesha kuwa inaingia dirisha dogo kwa utulivu, ikilenga kuongeza ubora bila kufanya mabadiliko makubwa ambayo yanaweza kuvuruga muundo wa kikosi chao.

The post SIMBA WAFICHUA MIPANGO YA DIRISHA DOGO appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/CHnNtmu
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post