KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Gocalves ameanza kufanya yake mapema baada ya kuyawasilisha maagizo rasmi kwa uongozi juu ya maboresho anayoyahitaji katika dirisha dogo la usajili.
Ripoti hiyo imeelezwa kuwa na maelezo ya kina juu ya maeneo yanayohitaji nguvu upya kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa uongozi chini ya Rais Hersi Said unatarajiwa kuketi kikao kizito cha bajeti ya usajili ndani ya siku chache zijazo. Kikao hicho ndicho kitakachotoa uamuzi wa mwisho juu ya majina ya wachezaji wanaoweza kuongezwa kwenye kikosi cha mabingwa hao watetezi.
Dirisha dogo linatarajiwa kufunguliwa Desemba 16 na kufungwa Januari 15, 2026, Yanga wanakesha kuhakikisha hawakosi watakowahitaji. Kwa kawaida dirisha hili huwa fupi na la ushindani mkubwa, klabu inakimbizana na muda ili ikamilishe mpango kabla ya timu nyingine kuvamia wachezaji wanaotakiwa.
Chanzo chetu kimedokeza kuwa ripoti ya Pedro si ya mabadiliko makubwa sana, bali imejikita zaidi katika kuyasafisha maeneo machache yenye udhaifu ambayo yamekwamisha timu kwenye baadhi ya michezo.
Pedro anatajwa kutaka kuongeza ubora katika nafasi mbili au tatu ambazo zimekuwa na upungufu katika miezi ya hivi karibuni.
“Tayari ripoti ya Pedro iko mezani kwa uongozi, na bajeti yake itajadiliwa ndani ya wiki hii,” kilisema chanzo chetu.
Inaelezwa kuwa mkakati wa ndani unataka kila kitu kikamilike mapema ili kocha awe na nafasi ya kuwapokea wachezaji wapya kabla ya kurejea kwa ligi hatua ya moto.
Mtoa habari huyo alifafanua kuwa lengo la ripoti hiyo ni kuongeza uhai wa kikosi, bila kufanya mabadiliko makubwa ambayo yanaweza kuvuruga muunganiko uliopo. Pedro anataka wachezaji waliopo waongezwe nguvu, hasa katika eneo lenye ushindani mdogo na lililoonyesha kusuasua katika mechi kadhaa.
“Baada ya kikao cha Jumamosi tunatarajia kupata mwanga zaidi. Pia kocha anafuatilia mastaa watakaong’ara AFCON ili kuona kama kuna wanaoweza kuongezwa,” amesema chanzo hicho.
The post PEDRO AUWASHA MOTO YANGA, AKABIDHI RIPOTI NZITO appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/KWeAzCB
via IFTTT
Post a Comment