MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameweka wazi kuwa mchakato wa kumpata kocha mkuu mpya wa timu hiyo upo mikononi mwa uongozi wa juu wa klabu kupitia bodi ya wakurugenzi, ambao wanashughulikia majina ya makocha walioomba au kupendekezwa kwa ajili ya nafasi hiyo.
Akizungumza kuhusu tetesi zinazomhusisha kaimu kocha wa Timu ya Taifa Stars na kocha wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi, Ahmed amesema hana taarifa zozote zinazothibitisha kama kocha huyo ameomba kazi au anatajwa rasmi kujiunga na Simba.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa jina la Gamondi limo kwenye orodha ya makocha wanaojadiliwa na bodi ya wakurugenzi wa Simba, kutokana na uzoefu wake mkubwa wa soka la Afrika na uelewa wake wa mazingira ya ligi za ndani na kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, Simba iliwahi kuwasilisha ofa rasmi kwa Singida Black Stars kwa lengo la kumchukua Gamondi, lakini uongozi wa klabu hiyo inayojulikana kama Walima Alizeti ulikataa ofa hiyo licha ya kuwepo kwa taarifa kuwa kocha huyo alikuwa na nia ya kujiunga na Wekundu wa Msimbazi.
Ahmed amesema kuwa yeye binafsi hana taarifa za kina kuhusu Gamondi kwa sasa, kwani mchakato mzima wa kumpata kocha mpya unasimamiwa na viongozi wakuu wa klabu, huku idara yake ikihusishwa baada ya maamuzi ya mwisho kufanyika.
Ameongeza kuwa mchakato huo unaendelea vizuri na matarajio ya uongozi ni kumpata kocha mkuu mapema, ili ifikapo Desemba 28 timu itakaporejea kambini, kocha huyo awe tayari ameshapatikana na kuanza kazi.
“Kuhusu Gamondi, hiyo ni taarifa mpya kwangu. Jukumu hilo liko kwa bodi ya wakurugenzi chini ya kamati ya mashindano, na baada ya mchakato kukamilika, nitapewa jina la kocha mpya ili nimtangaze rasmi kwa umma,” amesema Ahmed.
The post MAZITO KUHUSU GAMONDI, AHMEDY AFUNGUKA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/OwxDeW9
via IFTTT
Post a Comment