KOCHA mkuu wa Yanga, Pedro Gonçalves, amesema bado anabeba mzigo mkubwa wa kuhakikisha kikosi chake kinarejea katika ubora wa juu, licha ya matokeo mazuri ambayo wamekuwa wakiyapata kwenye michezo ya hivi karibuni.
Pedro anasema anahisi deni kubwa la kulijenga upya jina la Yanga, ili iwe bora kuliko ilivyokuwa msimu uliopita.
Msimu wa 2025 ulikuwa na misukosuko ndani ya benchi la ufundi la Yanga baada ya kuondoka kwa kocha Miguel Gamondi, ambaye alikuwa ametengeneza kikosi imara kilichoonesha kiwango cha juu.
Baada ya Gamondi kuondoka, timu ilipitishwa kwa makocha wawili, akiwemo Saed Ramović na baadaye Hamdi Miloud aliyemaliza msimu kabla ya nafasi hiyo kumfikia Romain Folz. Hata hivyo, Folz hakudumu na hatimaye timu ikakabidhiwa kwa Pedro.
Pedro anasema kupitia rekodi na ubora wa Yanga ya msimu uliopita, anajiona kwenye mtihani mkubwa na anairudisha timu hiyo kwenye kiwango kile kile au hata kuifikisha juu zaidi.
“Mafanikio ya zamani yanaweka shinikizo, lakini pia yanaipa hamasa ya kuongeza ubunifu na mbinu mpya ndani ya kikosi.
Ubora wa Yanga ya msimu uliopita unanipa picha ya kile kinachotakiwa kufikiwa, kazi yangu si tu kushinda mechi, bali kuijenga timu yenye utambulisho thabiti na uwezo mkubwa wa ushindani, msimu uliopita ulikuwa na viwango vinavyohitaji kufikiwa upya kwa jitihada za ziada,” amesema.
Pedro ameongeza kuwa licha ya timu kutofanya vizuri kimataifa, bado walionesha upinzani mkubwa na kuendelea kutetea mataji yao ya ndani, likiwemo taji la Ligi Kuu Tanzania Bara. Hali hiyo inaonyesha kuwa msingi wa timu bado upo imara na unahitaji kupangwa upya kwa umakini.
Kuhusu mabadiliko ya kikosi katika kila mchezo, Pedro amefafanua kuwa hajafanya hivyo kwa bahati mbaya, bali kwa ajili ya kupumzisha wachezaji waliocheza dakika nyingi msimu mzima.
Ameeleza kuwa ni muhimu kuwasawazisha wote kwa kuwapa nafasi wale ambao hawajapata muda wa kutosha ili kuongeza ushindani ndani ya timu.
Ameongeza kuwa wachezaji waliokuwa majeruhi sasa wanaanza kurejea taratibu, wanahitaji kupewa dakika chache katika michezo ili kurudisha utimamu wa miili yao. Lengo ni kuhakikisha kila mchezaji anakuwa fiti kwa ajili ya mechi zijazo.
Akizungumzia ugumu wa kupata ushindi katika mchezo dhidi ya Coastal Union, Pedro amesema hali ya uwanja ilikuwa changamoto kubwa kwao,
Amesisitiza kuwa “…inawezekana wenyeji wameuzoea.” Hata hivyo, ameahidi kuendelea kupambana ili kuhakikisha Yanga inapata matokeo bora bila kujali mazingira.
The post MATESO YA GAMONDI YANAMTESA PEDRO KWA YANGA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/eD6rjow
via IFTTT
Post a Comment