HAMZA AFANYIWA UPASUAJI, SIMBA YAPATA TUMAINI

BEKI wa kati wa Simba, Abdulrazack Hamza, hatimaye amekamilisha matibabu ya upasuaji yaliyofanyika nchini Morocco, hatua inayompa matumaini mapya ya kurejea uwanjani baada ya kipindi kirefu cha kuwa nje ya majukumu ya timu.

Uongozi wa Simba umethibitisha kuwa mchezaji huyo anaendelea vizuri na kwamba taratibu za mwisho za matibabu wa jeraha lake zinaendelea kufuatiliwa kwa karibu.

Hamza alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeraha yaliyomsumbua msimu huu, hali iliyoathiri mchango wake ndani ya kikosi cha wekundu wa Msimbazi.

Majeraha hayo yaliyokuwa yakijirudia yalimlazimu kufanyiwa vipimo vya kina ambavyo vilionyesha kuwa upasuaji ulikuwa hatua sahihi zaidi ili kurejesha ubora wake.

Kwa mujibu wa taarifa ya Simba, upasuaji huo umefanyika kwa mafanikio nchini Morocco, eneo ambalo klabu hiyo imekuwa ikitumia kwa wachezaji wake kupata huduma bora za kitabibu kutokana na ubobezi wa wataalamu wao.

Madaktari wamethibitisha kuwa beki huyo yupo katika hali nzuri na mwitikio wa mwili wake baada ya upasuaji unaridhisha.

Klabu imesema awamu inayofuata kwa mchezaji huyo ni kuanza programu maalumu ya itakayodumu kwa muda maalumu kabla ya kuruhusiwa kurejea kwenye mazoezi mepesi.

Ratiba yake ya kurejea dimbani itategemea mwendelezo wa maendeleo yake katika kipindi hiki cha kuimarika upya.

Hamza ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakitegemewa kwenye eneo la ulinzi kutokana na uthabiti, nguvu na utulivu wake katika kuongoza safu ya nyuma. Kutokuwepo kwake kumeifanya Simba kujaribu mbinu na muunganiko tofauti kwenye ulinzi msimu huu.

Kwa sasa mashabiki wa Simba wanapewa matumaini kuwa kurejea kwa Hamza kutaleta nguvu mpya, hasa katika kipindi ambacho timu inajiandaa na mechi ngumu za Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.

The post HAMZA AFANYIWA UPASUAJI, SIMBA YAPATA TUMAINI appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/HTnifJl
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post