YANGA imemaliza mechi mbili za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa nafasi ya pili katika msimamo wa kundi B, ikikusanya pointi nne iliposhinda dhidi ya FAR Rabat na sare kwa JS Kabylie, huku ikiwa imara katika safu ya ulinzi.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Yanga, upande wa Simba ambayo haina pointi katika Kundi D la michuano hiyo, inashika nafasi ya pili kwa umiliki wa mchezo.
Katika mechi hizo zote mbili, Yanga haijaruhusu nyavu zake kutikiswa na ni timu mbili tu ambazo hadi sasa hazijafungwa bao katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu. Nyingine ni Pyramids ya Misri.
Wakati mashabiki wa Yanga wakitambia makali yao kwenye mechi mbili zilizopita za Ligi ya Mabingwa Afrika, takwimu zinaonyesha nyota wawili wa kikosi chao ndio wamekuwa na mchango mkubwa zaidi katika kuifanya timu hiyo isipoteze mechi na kutoruhusu bao hadi sasa katika makundi.
Wachezaji hao ni kipa Djigui Diarra na Beki Ibrahim Abdullah ‘Bacca’.
Diarra anaongoza katika chati ya makipa waliocheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao na amefanya hivyo mara mbili.
Kipa huyo pia ana wastani wa asilimia mia moja wa kuokoa hatari na anashika nafasi ya tatu kwa kuokoa hatari katika dakika 90 na anaokoa wastani wa mashambulizi 3.5 kwa mechi.
Beki Ibrahim Bacca ndiye kinara wa kuondosha hatari ndani ya kikosi cha Yanga na katika mechi mbili zilizochezwa, amefanya hivyo mara 19 sawa na wastani wa mara 9.5 kwa mechi.
Kutoruhusu bao katika mechi mbili za mwanzo za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kumeifanya Yanga imalize nuksi ya muda mrefu ya kufungwa mabao katika mechi mbili za mwanzo za hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika.
Kabla ya hapo, hakuna msimu kati ya kumi iliyopita ambao Yanga ilicheza hatua hiyo iwe katika Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho Afrika bila nyavu zake kutikiswa.
Mbali na hayo, Celestine Ecua wa Yanga anashika nafasi ya kwanza kwa wachezaji waliopiga mashuti mengi yaliyolenga lango.
SIMBA UMILIKI JUU
Pamoja na kutoshinda mechi hata moja kati ya zile mbili za kwanza ambazo imecheza hatua ya makundi, lakini Simba imeonekana kuwa vizuri kumiliki mpira kwa muda mrefu ambapo wastani wake ni asilimia 62.1 kwa mechi ikiwa inashika nafasi ya tatu, nafasi ya pili inashikwa na RS Berkane yenye asilimia 64.6 na nafasi ya kwanza Mamelodi Sundowns ina asilimia 73.5 kwa kila mechi.
Pamoja na Simba kuonekana kuwa vizuri kwenye eneo hili, pia inaonekana kuwa kinara wa timu iliyopoteza nafasi nyingi kwenye michuano hii hadi sasa ikiwa inashika nafasi ya pili baada ya kupoteza nafasi tano za wazi hadi sasa, nafasi ya kwanza kwa timu iliyopoteza nafasi nyingi ni Esperance de Tunis ambayo pia ipo kundi moja na Simba, imepoteza nafasi nane, huku ya tatu ikishikwa na Berkane iliyopoteza nafasi tatu.
Kwa mujibu wa takwimu, Simba pia inashika nafasi ya tatu kwa timu ambayo imepiga mipira mirefu iliyofika kwa walengwa ikiwa imepiga wastani wa 34 kwa mechi, nafasi ya pili kwenye eneo hili ni Esperance de Tunis iliyopiga wastani wa 34.5, huku vinara ni Berkane iliyopiga wastani wa 38 kwa mechi.
Hata hivyo, pamoja na hayo yote Simba inaongoza pia kwa timu yenye nidhamu mbovu hadi sasa kwenye michuano hii ikiwa imekusanya jumla ya kadi tano, nne za njano na moja nyekundu, inafuatiwa na Saint-Eloi Lupopo yenye kadi tano za njano pamoja na Stade Malien tano.
TAKIMU ZINGINE
VINARA WA KUPIGA KONA
Al Ahly (15)
Saint-Eloi Lupopo (14)
Espérance (13)
VINARA WA PASI
Mamelodi Sundowns (566.0)
RSB Berkane (462.5)
Pyramids (434)
MASHUTI YALIYOLENGA LANGO KWA MECHI
Yanga (6.0)
JS Kabylie (5.0)
Stade Malien (4.5)
VINARA WA UFUNGAJI
Ahmed Atef El Sayed (Pyramids – 3)
Trezeguet (Al Ahly – 3)
Abdelrazig Omer (Al-Hilal – 2)
WALIOPIGA MASHUTI YALIYOLENGA LANGO
Celestin Ecua (Yanga – 3.0)
Trezeguet (Al Ahly – 2.5)
Aymen Mahious (JS Kabylie – 1.8)
The post DIARRA, BACCA ‘WAKICHAFUA’ HASWA CAF…..REKODI ZAO HAKUNA STAA WA SIMBA ANAZIFIKIA…. appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/hyk31ED
via IFTTT
Post a Comment