Viongozi wa Simba wameanza harakati za kukisuka kikosi hicho na tayari imeanza kuifukuzia saini ya beki wa Geita Gold, Samwel Onditi.
Onditi ambaye kwa sasa ni mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika, wawakilishi wake wamefanya mawasiliano na Simba huku ikielezwa kilichobaki ni kukubaliana maslahi. binafsi kwani mchezaji mwenyewe yupo tayari kujiunga nao.
Nyota huyo anayeweza kucheza kama beki na kiungo wa kati, alikuwa akiichezea Geita Gold iliyoshuka daraja msimu huu na kabla ya kujiunga na kikosi hicho cha mkoani Geita aliichezea pia Ihefu ambapo timu zote alizitumikia kwa mkopo kutokea Azam FC.
KLABU ya Azam imeanza mazungumzo ya kimyakimya na mabosi wa Zesco ya Zambia ili kumpata kipa, Ian Otieno kwa ajili ya msimu ujao.
Mabosi wa Azam wamefikia uamuzi huo baada ya kutokuwa na uhakika wa kubaki kwa kipa wa sasa wa kikosi hicho, Mohamed Mustafa aliyesajiliwa kwa mkopo Januari akitokea Al-Merrikh.
IMEELEZWA kwamba, kipa namba moja wa Tabora United, John Noble raia wa Nigeria, amezivutia timu nyingi za Ligi Kuu Bara ikiwemo KMC, baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika msimu wake wa kwanza kucheza Tanzania akitokea Enyimba ya Nigeria. Kipa huyo ambaye mkataba wake na Tabora United unamalizika Juni 30, mwaka huu, katika ligi ameweka ‘clean sheet’ 9.
KATIKA kuhakikisha msimu ujao inafanya vizuri zaidi, Simba Queens imeanza mazungumzo ya kumnunua moja kwa moja winga wa JKT Queens, Winifrida Gerald anayemaliza mkataba mwishoni mwa mwezi huu.
Ikumbukwe msimu huu, Simba ikifanikiwa kuchukua ubingwa wa WPL itashiriki mashindano ya kimataifa.
MABOSI wa Singida Black Stars zamani Ihefu, wameingilia kati dili la kiungo wa Tabora United, Najim Mussa. Staa huyu amekuwa katika kiwango bora msimu huu huku akiwaniwa na timu mbalimbali zikiwemo za Simba na Azam FC ila Singida pia imeingilia kati dili hilo kwa kile kinachoelezwa ni baada ya vigogo hao kupunguza kasi ya kumhitaji.
MSHAMBULIAJI wa Mashujaa, Athuman Masumbuko ‘Makambo Jr’ amepanga kuachana na timu hiyo baada ya kutokuwa na msimu mzuri kikosini humo. Nyota huyo alijiunga na Mashujaa msimu uliopita wa 2023/2024 baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiichezea timu ya vijana ya Mtibwa Sugar.
KLABU za Kariakoo, Simba Queens na Yanga Princess zimegonga hodi kwa Fountain Gate Princess kutaka saini ya kiungo Mkenya Involata Mukoshi ambaye anamaliza mkataba na matajiri hao wa Dodoma.
Mbali na Simba na Yanga pia inaelezwa Police Bullets ya nchini kwao Kenya ni kati ya timu zinazomfuatilia ili aweze kuongeza nguvu kwenye klabu hiyo.
Post a Comment