Klabu ya Yanga imesema kuwa inasubiri ripoti ya kocha wao mkuu, Miguel Gamondi kwa ajili ya kufanya maamuzi ni wachezaji gani waachwe na wachezaji gani waongezwe kwenye kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao.
Hayo yamesemwa na Meneja habari wa Klabu hiyo, Ally Kamwe wakati akizungumza kuhusu kuelekea usajili mpya wa msimu ujao huku akisisitiza kuwa nyota wao wanaowahitaji hawataruhusu waondoke hata kama ni biashara.
“Kama ambavyo alizungumza Rais wa Klabu yetu, Eng. Hersi Said, wachezaji wote ambao ripoti ya kocha wetu Miguel gamondi itakuwa imeelekeza wabaki, watasalia kwenye klabu yetu. Yanga tupo kwenye level ya juu ya weredi, unapokea ripoti ya kocha kisha viongozi wanakuja kufanya tathmini.
“Kwa hiyo wale ambao kocha atawahitaji kwa ajili ya msimu ujao, watasalia hapa, huwezi kuwa na maono ya kutawala soka la Afrika halafu kila msimu tukawa tunakubali kuachia wachezaji wetu bora. Tunafahamu soka ni biashara lakini pia klabu ina malengo yake. Kwa hiyo lazima biashara iendane na malengo ya klabu.
“Malengo yetu ya msimu ujao tumeshayaainisha ni kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa hasa Klabu Bingwa Barani Afrika, achana na haya ya ndondo cup. Kuyafikia haya malengo lazima tuhakikishe tunasalia na wachezaji wetu bora na tunaongeza nguvu,” amesema Kamwe.
Post a Comment