Timu ya Wydad Casablanca imeonyesha nia ya kumsajili kipa wa Simba, Ayoub Lakred kwa ajili ya msimu ujao.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zimeliambia Mwanaspoti kwamba nyota huyo raia wa Morocco anataka kuondoka msimu ukiisha baada ya mkataba wake wa mwaka mmoja kumalizika jambo linalowatia wasiwasi mabosi wa Simba wanaomtaka abaki.
Lakred aliyejiunga na Simba Agosti 12, mwaka jana akitokea FAR Rabat ya Morocco akisaini mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine, amekuwa mhimili muhimu tangu alipoumia kipa namba moja, Aishi Manula jambo lililowashtua mabosi endapo ataondoka hali itakuwaje. Mtu wa karibu na mchezaji huyo amebainisha kwamba Lakred baada ya kupata ofa ambayo kwake anaiona ni nzuri anafikiria kuondoka na kusitisha kuongeza mwaka mwingine kubakia Msimbazi kwani anataka kurudi kwao akiamini ni sehemu salama kwa sababu ni nyumbani na ndipo ilipo familia yake.
“Mbali na kutaka kurudi nyumbani pia ofa aliyoipata kutoka Wydad ni kubwa na hayupo tayari kuiacha. Kwa viongozi wa Simba ukiwasikiliza wanakwambia bado wanahitaji kubaki naye kwa sababu ameonyesha kiwango kizuri,” amesema mtu huyo.
Naada ya mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba dhidi ya Azam uliochezwa Alhamisi iliyopita, Lakred alionekana akiwa na mkewe na chanzo chetu kinaeleza mwanamke huyo amevutiwa na mazingira ya Tanzania jambo ambalo huenda likabadili msimamo wa kipa huyo kuondoka.
“Mke wake amefurahia sana mazingira ya hapa (Tanzania), hiyo imetokana na jinsi alivyoona mume wake anashangiliwa. Hivyo alipendezwa na hali hiyo, ni faida nyingine ambayo Simba inaweza kunufaika nayo japo uamuzi wa mwisho ni wa mchezaji,” kilisema chanzo hicho.
Katika taarifa ya Simba wakati inamsajili ilieleza amesaini mkataba wa miaka miwili, lakini Mwanaspoti linafahamu kwamba alisaini hadi mwisho wa msimu kukiwa na kipengele cha kuongezewa mwingine.
Katika mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu Lakred amecheza 13 kwa dakika 1170 akiwa hajaruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba. Kipa huyo aliyezaliwa Juni 1995 mbali na kuichezea FAR Rabat, timu nyingine aliyoichezea ni RS Berkane zote za Morocco na alisajiliwa ikiwa ni muda mfupui tangu Simba ilipoachana na Mbrazili Jefferson Luis.
Simba iliachana na Jefferson iliyemsajili kutoka Resende ya Brazil huku akiwa hajacheza mchezo wowote baada ya kugundulika ana majeraha ya misuli wakati timu hiyo ikiwa Uturuki ilipoweka kambi ya maandalizi ya msimu huu.
UMUHIMU WAKE SIMBA
Wakati hayo yakiendelea ndani ya Simba, kipa huyo amefanikiwa kuziba kwa usahihi pengo la Manula aliye nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Lakred amefanikiwa kuwaaminisha mashabiki wa timu hiyo kwamba wasiwe na wasiwasi licha ya Manula kukosekana kwani hapo awali ilikuwa ikionekana kwamba amekosekana Manula goli, waliopo walishindwa kuvaa viatu vyake kwa usahihi, lakini sasa hakuna mashaka hayo.
Manula aliyejiunga na Simba Agosti 9, 2017 akitokea Azam FC, ameonyesha kiwango bora muda wote na pindi alipokosekana waliokuwepo walishindwa kupindua ufalme wake ndani ya timu hiyo.
Baadhi ya makipa waliojiunga na Simba na wakashindwa vita na Manula ni Beno Kakolanya aliyetokea Yanga 2019 akiwa katika kiwango bora, Said Mohamed ‘Nduda’ alitokea Mtibwa Sugar na Deogratius Munishi ‘Dida’ aliyerejea kwa mara ya pili.
Dida alirejea katika kikosi hicho 2018 ikiwa ni msimu wake wa pili akitokea Afrika Kusini katika Klabu ya Chuo cha Pretoria ‘Tucks FC’ huku kipa mwingine aliyeshindwa vita hiyo ni Emmanuel Mseja aliyesajiliwa Simba akitokea Mbao FC. Vilevile Jeremiah Kisubi aliyetua Msimbazi akitokea Julai 2, 2021 akitokea Tanzania Prisons.
Kwa sasa Simba wapo makipa wengine wazuri wakiongozwa na Hussein Abel na Ally Salim ambao wamekosa nafasi ya kucheza mara kwa mara, hivyo kutoa nafasi zaidi kwa Lakred ambaye amekuwa panga pangua.
Manula ameonyesha uwezo mkubwa na kuitwa ‘Tanzania One’ siyo kwa bahati mbaya kwani tangu ajiunge na Simba ametwaa mataji mengi yakiwemo ya Ligi Kuu Bara manne mfululizo misimu ya 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021.
Mbali na hayo pia amechukua tuzo nyingi binafsi huku akiiwezesha Simba kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara tano kati ya sita iliyoshiriki huku mara moja ikiwa ni Kombe la Shirikisho la Afrika.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Lakred amecheza mechi tisa kuanzia hatua ya mtoano huku Manula akidaka moja.
No comments:
Post a Comment