Kikosi cha Yanga kinaondoka leo Alhamisi jijini Dar es Salaam kwenda Lindi ili kuwahi pambano la Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi akianika faili la kiungo mshambuliaji, Maxi Nzengeli ambaye hajaonekana kwenye mechi mbili zilizopita.
Yanga itavaana na Namungo kesho Ijumaa kwenye Uwanja wa Majaliwa, uliopo Ruangwa ikiwa inarudi kwenye Ligi Kuu ikitokea katika majukumu ya mechi za kimataifa ikifuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini Kocha Gamondi akifichau sababu za kutoonekana uwanjani kwa Maxi mwenye mabao manane hadi sasa katika ligi hiyo.
Kocha huyo raia wa Argentina alisema, Maxi ameshindwa kuitumikia timu hiyo kwa vile ni majeruhi akiwa ameumia mkono, huku akikiri kukosekana kwake kumeiyumbisha timu hiyo kwani ni mmoja ya nyota tegemeo.
Maxi aliumia katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya CR Belouizdad wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 4-0 na kufuzu robo fainali kabla ya wikiendi iliyopita kwenda Misri kukamilisha ratiba dhidi ya watetezi wa taji hilo, Al Ahly na kulala bao 1-0 ugenini ambao Mkongoman huyo hakucheza.
Mbali na mechi hiyo, pia Maxi aliukosa mchezo wa 32 Bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Polisi Tanzania na Yanga ilishinda mabao 5-0 na mechi ya kesho itakuwa ni ya tatu kwake kuikosa kwani anaendelea kuugua mkono huo uliofungwa plasta ngumu ‘hogo’ (P.O.P).
“Siwezi kuacha kumtumia Nzengeli (Maxi) bila sababu ni mchezaji mzuri na ana mchango mkubwa kwa timu hakutumika kwa sababu ni majeruhi na bado anaendelea na matibabu alipata shida kwenye mkono uliofungwa POP,” alisema Gamondi aliyefafanua, anaheshimu mchango wa nyota huyo kikosini lakini hawawezi kulazimisha kumtumia wanahofia kumwongezea maumivu zaidi hivyo atakaa nje ya uwanja hadi atakaruhusiwa na daktari.
Akizungumzia msafara unaoondoka leo kuifuata Namungo tayari kwa mchezo wa Ijumaa, Gamondi alisema jana jioni walikuwa wanaendelea na maandalizi kujiweka fiti kabla ya safari na wapo tayari kwa ajili ya kuendeleza mapambano.
“Tunaenda kwa kumheshimu mpinzani tunatarajia ushindani lakini tumejiandaa kusaka pointi tatu muhimu ambazo zitaendelea kutupa uongozi na kurudisha morali ya wachezaji baada ya kupoteza mchezo wetu wa mwisho dhidi ya Al Ahly,” alisema.
Yanga wanakwenda huko wakiwa na faida ya kushinda mchezo wa mwisho dhidi ya Namungo kwa bao 1-0 lililofungwa na Mudathir Yayha, hivyo utakuwa ni mchezo wa kisasi.
Matokeo ya Namungo akiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani kwenye mechi za hivi karibuni kati ya mechi tano wameshinda nne na kufungwa mchezo mmoja wamefunga mabao saba na kufungwa matatu.
Wakati Yanga kwenye mechi zake za ugenini kwa michezo ya hivi karibuni kati ya mitano wameshinda mitatu, sare moja na kufungwa mchezo mmoja.
PATA GB 30 KILA MTANDAO BURE HAPA
No comments:
Post a Comment