Mabosi wa Simba wajanja sana, wakati wakiendelea na mikakati kuhakikisha timu hiyo inafanya kweli mbele ya Al Ahly ya Misri katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tayarwameanza usajili wa kimyakimya na kwa sasa wanamalizana na beki mmwaga maji wa Al Hilal ya Sudan.
Simba inayojiandaa kushuka uwanjani Ijumaa, inadaiwa imeanza mazungumzo na beki wa kushoto wa zamani wa mabingwa hao wa Sudan walioomba kuja kucheza Ligi Kuu Bara, Ibrahim Imoro anayesifika kwa kukaba na kupandisha timu na kupiga krosi za maana kwa washambuliaji wa timu hiyo.
Chanzo makini kutoka ndani ya Simba kinasema beki huyo Mghana anatakiwa kutua Msimbazi ili kuja kusaidiana na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye kwa muda mrefu hana mbadala kikosini katika eneo hilo la kushoto na mazungumzo yapo katika hatua nzuri kwa sasa na mambo yakienda sawa atatua Msimbazi.
Imoro anayemudu pia kucheza kama winga wa kushoto, kwa sasa yupo huru baada ya kuvunja mkataba na Al Hilal iliyomsajili Agosti 5, 2022 kutoka Asante Kotoko ya Ghana tangu Julai mwaka jana na tayari ameshaanza mazungumzo na mabosi wa Msimbazi ili aje kuitumikia msimu ujao.
Mghana huyo mwenye umri wa miaka 24 amewahi kutwaa Tuzo ya Mchezaji aliyeasisti mabao mengi katika Ligi ya Ghana msimu wa 2021-2022 akitoa pasi tisa, pia ametwaa mataji zaidi ya manne ikiwamo la Ligi Kuu Ghana akiwa na Asante Kotoko msimu wa 2021-2022 na Kombe la Rais (Ghana) 2019 na taji la Sudan Super Cup 2022 akiwa na Al Hilal.
MSIKIE MWENYEWE
Mwanaspoti lilimtafuta beki huyo ili kujua ukweli wa taarifa huyo ambapo alikiri ni kweli amekuwa akizungumza na klabu kadhaa za Tanzania ikiwamo Simba baada ya awali Azam nao kumhitaji lakini dili likashindikana.
Alisema kwa mchezaji yeyote anayejitambua kuhitajiwa na klabu kubwa kama Simba sio kitu cha kupuuza kwani hata yeye anatamani kuvaa uzi wa Wekundu hao baada ya kuvunja mkataba mapema na Al Hilal ili awe huru kwenda kokote bila kubanwa na kukiri Simba ipo hatua nzuri kumbeba.
“Niliamua kufanya hivyo (kuvunja mkataba) ili dili langu likikamilika kusiwe na kikwazo tena, kwa sasa kama ishu yangu na Simba ikikamilika itakuwa ni hatua kubwa sana. Ninachosubiri ni kumalizana nao na kama kila kitu kitakuwa sawa basi msimu ujao nitaanza majukumu yangu mapya nikiwa na jezi nyekundu,” alisema Imoro.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Simba, Ahmedy Ally alisema; “Simba ni taasisi kubwa kwa sasa akili zetu wengi zipo kwenye mchezo ujao ambao ni mgumu dhidi ya Al Ahly, lakini mchezo huu hauzuii majukumu mengine kuendelea.”
Ahmed aliongeza kwa kusema; “Sote tunafahamu wachezaji bora kama Imoro sio taarifa mbaya kuhusishwa na klabu kubwa kama Simba, lakini itoshe tu kusema hilo kama lipo litakuja kuwa wazi kwa wakati muafaka na umma na Simba utajulishwa kama taarifa nyingine za usajili tunavyoziweka wazi.”
Rekodi zinaonyesha Imoro aliyekuwa akipata nafasi ya kikosi cha kwanza cha Florent Ibenge, katika mechi sita za mwisho za Hilal alitumika kwa dakika 482, huku mchezo mmoja pekee ndio amecheza dakika 32 tu.
Kabla ya kuibuka kwa taarifa za Imoro, Simba ilielezwa pia ilituma maombi ya kutaka kumsajili straika wa Azam FC aliyevunja mkataba, Prince Dube ikiwa sambamba na Al Hilal ambayo kwa sasa ipo kambini Cairo, Misri ikisikilizia dili la kutaka kuja kucheza katika Ligi Kuu Bara msimu ujao.
PATA GB 30 KILA MTANDAO BURE HAPA
No comments:
Post a Comment