Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Chama cha watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wameitaka klabu ya Simba kuomba radhi kwa tukio waliloita la udhalilishaji
Tukio hilo lilitokea Agosti 6, 2023 kwenye sherehe ya tamasha la siku ya Simba lililofanyika uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam kwa kumpandisha mtu mwenye ulemavu wa ngozi akiwa amevishwa taulo ya watoto (baby diaper)
Akizungumza leo Jumatano Agosti 9, 2023 jijini Dar es Salaam mwenyekiti wa TAS, Godson Mollel amesema tukio hilo ni la pili kwa Simba kulifanya ambalo la kwanza lilikuwa Agosti 8, 2022 waliingia na jeneza ambalo lilimbeba mtu mwenye ualbino
Amesema vitendo hivyo vinawatweza utu wa watu wenye ualbino nchini na kupelekea kuwepo kwa mijadala mingi katika jamii ikiwemo mitandaoni inaonyesha dhihaka kwa watu hao kinyume na haki za binadamu
Mollel amesema kwa miaka mingi kumekuwa na jitihada kubwa za utetezi wa watu wenye ualbino nchini kutokana na historia ya madhila yaliyopelekea watu hao kupoteza maisha,pamoja na idadi kubwa ya wahanga wa vitendo vya ukatili na unyanyapaa
"Tunasisitiza utani wa jadi uliopo wa Simba na Yanga hauhalalishi vitendo vya kutweza utu wa mtu kwa sababu yoyote ile iwe kwa kukusudia ama kwa kutokukusudia," amesema Mollel
Pia, amesema jamii nyingi watu wenye ualbino wamekuwa wakihusishwa na mila na tamaduni mbaya zinazotweza utu wao, hivyo kuendelea kwa vitendo hivyo ni kudididmiza juhudi za serikali, Mashirika watetezi na wadau binafsi za kuelimisha jamii kuhusu ualbino.
Amesema vitendo vya namna hii vinaporuhusiwa kufanywa hususani na taasisi kubwa ya Simba yenye ushawishi kwa jamii inarudisha nyuma kwa kiasi kikubwa jitihada zote zinazofanywa katika kuhamasisha taswira chanya za watu wenye ualbino
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Anna Henga ametoa rai kwa taasisi zote zenye ushawishi katika jamii hususani timu kubwa za mpira wa miguu kuepukana na vitendo vyenye sura ya udhalilishaji na badala yake wajikite katika kuhamasisha heshima na utu
Henga amewataka watu wenye ualbino kutochukulia vitendo vya aina hiyo kwa wepesi na badala yake kuvikemea vikali kwa maana na wao ni binadamu kama wengine wenye haki ya kutodharirishwa na kuheshimiwa na utu wao
Pia amewataka uongozi wa Simba kuomba radhi kwa watu wenye ualbino na umma kwa vitendo vya kutweza utu wao,na kuiomba Serikali pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) kusimamia jambo hilo
Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment