Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Hatimaye Uongozi wa Simba SC umetoa ufafanuzi wa kina namna utakavyomuaga kwa heshima Jonas Mkude, waliyeachana naye juma lililopita.
Simba SC imepanga kumuaga Mkude kwenye tamasha la Klabu hiyo ‘Simba Day’ litakalofanyika mwezi Agosti, mbele ya Mashabiki na Wanachama ambao hukusanyika kwa pamoja Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Siku chache baada ya Simba SC kutangaza kuachana na Mkude aliyemaliza mkataba wake, Kiungo huyo mkongwe anahusishwa kujiunga na Young Africans kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Afisa habari wa Young Africans Ally Kamwe juzi Alhamis (Juni 29) alinukuliwa akisema klabu hiyo hawatamruhusu mchezaji ambaye wamemsajili kwenda katika klabu aliyotoka kwa ajili ya kuagwa kwa heshima kauli ambayo ilitafsiriwa kumlenga Mkude waliyemsajili.
Meneja wa Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally amesema watakachokifanya uongozi wa klabu hiyo ni kutoa mualiko kwa mchezaji huyo kama ilivyokuwa kwa wachezaji waliopita ambao waliagwa kwa heshima kwenye tamasha hilo.
Amesema huo utakuwa mualiko kwa mchezaji husika licha ya kuajiriwa na klabu nyingine wao wanachokiangalia nini walichokipanga kuhakikisha wanatimiza lengo lao la kumuaga nyota huyo kwa heshima kubwa.
“Sisi tutamualika Mkude tu, kuhusu mwajiri wake kumruhusu au kutomruhusu hilo juu yao, tutatimiza kile tulichokipanga kwa mchezaji wetu huyo, tamasha letu lililopita tulimualika Maddie Kagere ambaye alikuwa tayari ameshapata timu, Taddeo Lwaga alikuwa amesajiliwa na klabu ya Djibouti na wote waliruhusiwa wakaja na kuagwa kwa heshima,” amesema Ahmed.
Amesema maamuzi ya kuhudhuria tamasha hilo na kupokea heshima yake ipo mikononi mwa mchezaji huyo na uongozi wake mpya.
Mkude ndiye aliyekuwa mchezaji mkongwe zaidi ndani ya klabu ya Simba SC baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka 13 akitokea timu ya vijana.
Katika hatua nyingine, Ahmed amesema wanasubiri kalenda mpya ya mashindano ya Shirikisho la soka nchini (TFF) ili kujua lini hasa wataanza maandalizi ya msimu mpya.
“Hatuwezi kusema ni lini tutaingia kambi au kufanya maandalizi ya msimu wa 2023/24 hadi hapo tutakapopata kalenda yaTFF ya msimu ujao, maana unaweza kuingia kambini Julai hii kumbe ligi inaanza Septemba, tunasubiri TFF wakishatoa kalenda yao tu na sisi tunaanza sasa maandalizi yetu na ndio hapo tutajua tunaenda kuweka kambi wapi japo taarifa za awali tutaenda Uturuki,” amesema Ahmed.
Pia Ahmed amegusia suala la kiungo wao Sadio Kanoute ambapo amesema nyota huyo bado yupo sana ndani ya kikosi cha timu hiyo baada ya kutoonekana muda mrefu hasa katika michezo ya mwisho ya ligi msimu uliopita.
“Tukumbuke mkataba wa Kanoute umebaki mwaka mmoja na yupo sana Simba SC, wachezaji ambao wamemaliza mkataba na wako katika mazungumzo ya kumuongeza ni Shomari Kapombe na Mohammed Hussein ambao muda wowote wataongeza na kusalia ndani ya kikosi cha Simba SC na kucheza Super League” amesema Ahmed.
No comments:
Post a Comment