Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba, amesema mafanikio iliyopata Klabu ya Yanga kwa kufika fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika msimu huu yanapaswa kuwa darasa kwa watani wao wa jadi, Simba.
Alitoa kauli hiyo jana bungeni jijini hapa alipowasilisha taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24.
Waziri huyo aliipongeza Yanga kwa kutinga fainali ya michuano hiyo na kutoa mfungaji bora (Fiston Mayele) na kipa bora (Djigui Diarra).
“Hakika Timu ya Simba mna mengi ya kujifunza kutoka Timu ya Yanga. Na timu zingine zijifunze ili mwaka kesho tuwe na timu nyingi zinazofanya vizuri kama Simba na Yanga walivyofanya vizuri mwaka huu,” alisema.
Aliipongeza Klabu ya Simba kwa kuendelea kufanya vizuri kimataifa na kufikia hatua ya robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Waziri huyo pia alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta hamasa kwa timu hizo katika michezo ya kimataifa kwa kununua kila goli linalofungwa katika mashindano hayo, Simba imepata jumla ya Sh. milioni 55 na Yanga Sh. milioni 135.
Pamoja na hayo, alisema mafanikio mengine ni timu ya mpira wa miguu ya watu wenye ulemavu (Tembo Worriors) iliyofuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia kwa Watu Wenye Ulemavu na kuiweka nchi katika orodha ya timu 10 bora za dunia na Timu ya Taifa ya Wanawake (Serengeti Girls) iliyoshiriki fainali za Kombe la Dunia huko India na kufikia hatua ya robo fainali mwezi Oktoba mwaka jana.
Alisema kwa kipindi hicho Tanzania pia kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 44 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) mwaka 2022 uliofanyika jijini Arusha na Mkutano wa Kimataifa wa Mawaziri wa Michezo wa Baraza la Michezo la Afrika Kanda ya IV uliofanyika jijini Arusha.
Tanzania ilichaguliwa kuwa Makao Makuu ya Sekretarieti ya Baraza hilo.
“Pia Tanzania imewasilisha zabuni ya kuomba kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2027 kwa ushirikiano na nchi za Kenya na Uganda,” alisema.
Pia alisema imetolewa mikopo kwa awamu mbili yenye thamani ya Sh. Bilioni 1.07 kwa wasanii na wadau 45 katika tasnia za utamaduni na sanaa.
Mwigulu pia alisema serikali imeratibu matamasha mbalimbali yenye lengo la kudumisha urithi wa utamaduni ikiwamo kuandaa na kuendesha mashindano ya Kimataifa ya Urembo na Utanashati kwa Viziwi mwaka 2022 ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika barani Afrika.
Chanzo: Dar24
Post a Comment