Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, wanaweza kupata wakati mgumu kukataa ofa ya Randi milioni 22 (Sawa na Sh 2,806,936,000) kwa ajili ya kumuachia mshambuliaji wao kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele kujiunga na Sepahan SC ya nchini Iran.
Mayele amekuwa katika kiwango bora kwa misimu miwili aliyoitumikia Young Africans ambapo msimu wa 2022/23 ametangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara.
Mkongomani huyo mbali na kuwa Mchezaji Bora, pia alitangazwa kuwa Mfungaji Bora akifikisha mabao 17 sawa na kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Mrundi Saido Ntibazonkiza, huku pia akitwaa Tuzo ya Bao Bora na kuingia katika kikosi bora cha Ligi Kuu Bara.
Mtandao mmoja kutoka Afrika Kusini, umeripoti jumla ya klabu tatu zimeonesha nia ya kuhitaji saini ya mshambuliaji huyo ikiwemo Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Mtandao huo ulizitaja klabu nyingine zinazomuhitaji Mayele ni Sepahan SC, Al Hilal ya Sudan na Hatta ya UAE ambazo zote zimemfuata meneja wa mchezaji huyo kwa ajili ya kufanya mazungumzo.
Klabu hizo zinapata ugumu kutokana na mkataba wa mwaka mmoja alionao Young Africans, ambao ameusaini katikati ya msimu uliomalizika.
Licha ya mkataba huo, lakini meneja wa Mayele pamoja na uongozi wa Young Africans umesema upo tayari kusikiliza ofa kutoka kwa klabu hizo.
Rais wa Young Africans, Injinia Hersi Said, alibainisha kwamba: “Bado hatujapokea taarifa yoyote kutoka Afrika Kusini, na hakuna klabu hata moja iliyowasiliana nasi.”
Wakala wa Mayele, hivi karibuni alisema klabu pekee ya Afrika Kusini iliyoonesha nia ya kumtaka mshambuliaji huyo ni Mamelodi Sundowns.
No comments:
Post a Comment