Winga Geita gold anukia Simba - EDUSPORTSTZ

Latest

Winga Geita gold anukia Simba


 Simba imeanza harakati za kuimarisha kikosi chake na miongoni mwa nyota wanaotajwa kuwa katika mpango wa kuwanasa ni winga wa Geita Gold, Edmund John.


Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti limezipata zinasema tayari winga huyo mwenye umri wa miaka 20 ameanza mazungumzo na Simba kwa ajili ya kujiunga nayo msimu ujao.


Nyota huyo wa zamani wa Serengeti Boys, anamudu kucheza nafasi za winga zote mbili kulia na kushoto pia ana uwezo wa kucheza nafasi ya nyuma ya mshambuliaji.


Harakati za kumsajili Edmund zimeanza kutokana na mapendekezo ya Kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' ambaye katika ripoti yake ameutaka uongozi kusajili mawinga wawili wazawa wanaomudu kucheza kila upande.


"Mazungumzo yanaendelea baina ya Simba na mchezaji na yanakaribioa kufikia pazuri. Tunafahamu ana mkataba na Geita Gold hadi Januari mwakani lakini tunaweza kuzungumza nao na tukafikia mwafaka wala hakuna shida katika hilo."


"Kocha amependekeza tusajili mawinga wawili wazawa ambao wataleta ushindani kwa wageni na huyu Edmund ni miongoni mwa wachezaji wa nafasi hiyo walioonyesha kiwango kizuri msimu huu," alisema mmoja wa vigogo wa Simba.


Licha ya kucheza nafasi ya winga, Edmund ni miongoni mwa wachezaji wa nafasi hiyo walioonyesha uwezo wa kufumania nyavu msimu huu ambapo hadi sasa ameifungia timu yake mabao manne dhidi ya Tanzania Prisons, Dodoma Jiji, Polisi Tanzania na Coastal Union.


Wakati ikiwa katika mpango wa kumnasa winga huyo, Simba pia iko katika mpango wa kumwongezea mkataba winga wake kiraka Jimmyson Mwanuke ambaye mkataba wake wa miaka mitatu utafikia tamati mwishoni mwa msimu ujao.


Uwezo mkubwa wa Mwanuke kucheza nafasi tofauti uwanjani pamoja na nidhamu anayoonyesha vinatajwa kama sababu iliyomshawishi Robertinho kufanya maamuzi ya kuendelea kubaki na nyota huyo aliyesajiliwa kutokea Gwambina FC.


Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema timu yake haijafanya mchakato wa usajili wa Edmund na suala la Mwanuke kama lipo au halipo litatolewa ufafanuzi.


"Taarifa kuhusu Simba kumhitaji Edmund sisi wenyewe tunaziona tu kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, kuhusu Mwanuke kama kuna chochote klabu itatoa taarifa," alisema Ally.


Chanzo: MwanaspotiDownload our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz