Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Uongozi wa Simba SC umesema kwa sasa akili zao wanazielekeza kwenye michuano ya CAF Super League na tayari wameshaanza maandalizi ya michuano hiyo, ambayo kwa mara ya kwanza itaunguruma mwaka huu 2023.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema kuwa, wakati viongozi, watu wa skauti na makocha wakiangalia wachezaji wa kuwasajili, mazoezi yanayofanyika sasa ni maandalizi ya Super League pamoja na msimu mpya wa Ligi Kuu wa 2023/2024.
“Tayari tumeshaanza maandalizi ya msimu ujao, haya yanayoendelea ni maandalizi ya ajili ya mashindano yajayo pamoja na ligi kwa sababu msimu mpya unaanza hivi karibuni, kama tulivyosikia msimu utaanza kwa Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii itakayochezwa kwa mfumo wa timu nne msimu huu, kwa hiyo lazima tuanze maandalizi na michuano ya CAF msimu ujao itaanza mapema sana, tuko makini ndiyo maana tumeamua kuanza mipango mapema,” amesema Ahmed
Amesema pamoja na kwamba wachezaji wao wanaendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi mbili za mwisho wa Ligi Kuu, lakini makocha wanatumia muda huo huo kuandaa kikosi cha msimu ujao na kuangalia wachezaji wa kuendelea kufanya nao kazi.
“Kikosi chetu kinaendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi zetu mbili za mwisho, Polisi Tanzania Juni 6 na Coastal Union Juni 9, tangu ratiba ilivyosogezwa mbele kikosi kimeendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Mo Arena Bunju, dhamira yetu kushinda mechi zote mbili pamoja na kwamba sisi tumemaliza ligi, lakini mechi hizi zina thamani kubwa kwetu na mashabiki wetu,” amesema Ahmed.
Baada ya kukosa ubingwa wa Tanzania Bara kwa msimu miwili mfululizo, huku ikiishia Robo Fainali kwenye michuano ya kimataifa, wanachama na mashabiki wa Simba SC wamekuwa wakiwapigia kelele kwa viongozi wao kufanya usajili wa wachezaji wenye uwezo watakaowavusha walipofikia sasa.
Uongozi wa Simba SC tayari upo kwenye mchakato wa kusaka wachezaji wenye uwezo ili kuwasajili kujiandaa na msimu mpya.
Katika hatua nyingine, Ahmed amesema kocha wao msaidizi Juma Mgunda bado yuko sana ndani ya benchi hilo akisaidiana vizuri na bosi wake Roberto na wanatambua umuhimu na uwezo wa kocha huyo mzawa kwa kuwa ndani ya timu hiyo anaishi vizuri na wachezaji wa benchi zima la ufundi.
Kauli hiyo ya Ahmed imekuja siku chache baada ya kuzagaa taarifa zikimuhusisha kocha huyo kutimka ndani ya kikosi cha Simba SC.
“Mgunda yupo sana Simba SC, kutokuwapo hizi siku mbili katika mazoezi ni kwa sababu alikwenda kwao Tanga kwa ajili ya mapumziko mafupi na sasa amerejea na ameendelea na majukumu yake ndani ya kikosi cha timu yetu, wanaofikiri kuwa anaondoka watasubiri sana,” amesema Ahmed
No comments:
Post a Comment