Pluijm afunguka uanachama wake Yanga, amtaja Msuva - EDUSPORTSTZ

Latest

Pluijm afunguka uanachama wake Yanga, amtaja Msuva

Ofa ya Bando la Internet wiki BURE Bonyeza HAPA


Ajira Mpya zilizotangazwa leo Bonyeza HAPA


Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA

Aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Azam na sasa Singida Big Stars, Hans Pluijm ni wazi kila mmoja anajua aliwahi kuwa mwanachama wa klabu ya Yanga kwa wakati huo.


Pluijm alivyoondoka kwenda Singida United na baadaye Azam FC, wengi wao waliendelea kuamini kwamba kocha huyo bado mwanachama wa Yanga kutokana na awali kujisajili.


Spoti mikiki lilifanya mazungumzo na Pluijm kwenda hadi nyumbani kwake Singida, Mtaa wa Paradise na kufunguka mengi ikiwemo suala lake la uanachama Yanga pamoja na mipango yake ya sasa akiwa na Singida Big Stars.


Si mwanachama hai Yanga


Pluijm anasema huku akicheka, kuwa suala lake la uanachama Yanga lilishaisha muda mrefu kwa sababu alishasahau kabisa masuala ya kulipia kadi ambayo yanamfanya awe hai.


"Nilikuwa na kadi, lakini haikuendelea kuwa hai kwa sababu sikuwa nalipia, kwahiyo tayari mimi si mwanachama wa kule tena kwa muda mrefu sana.


"Lakini mashabiki wameendelea kuwa wema kwangu kwa sababu huwa wananitumia ujumbe wa kunisalimia nikiwa hapa na hata kabla sijaja kabisa huwa wananisalimia," anasema Pluijm.


Ukurugenzi wa ufundi wamshangaza


Pluijm akiwa na Yanga alichukua makombe matatu, Ligi Kuu, Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), lakini baadaye uongozi wa timu hiyo uliamua kumtema.


Kutemwa kwake Yanga haikuwa moja kwa moja, mabosi wa timu hiyo walimpeleka kuwa mkurugenzi wa benchi la ufundi kisha awe anahusika kwenye masuala mengine ya benchi hilo.


Lakini mwenyewe anafunguka na kusema nafasi hiyo akiwa Yanga hakuwahi kabisa kuielewa kwa sababu kwa upande wake hajawahi kuona akiitendea haki.


"Ilinishangaza sana kiukweli, mimi kwenda kwenye kile cheo nikiwa nimeifanyia vitu vingi timu, nilikuwa TD (Technical Director/Mkurugenzi wa ufundi), lakini sikuwahi kuwa hata na ofisi.


"Ukiwa mkurugenzi wa ufundi ni lazima utengeneze mfumo ambao utakuwa unaiongoza timu kwa muda mrefu kuanzia chini kwa vijana hadi juu, lakini kwangu nilikuwa nipo nipo tu," anasema Pluijm.


Yanga ya sasa na ile yake


Pluijm anainama kisha anacheka na kuweka wazi kabisa kwamba Yanga ambayo alikuwa kocha mkuu ilikuwa na wakati mgumu tofauti na ambavyo kwa sasa ipo.


"Yanga yetu kiukweli kila mmoja anajua ni namna gani ambavyo tulikuwa, uwanja wa mazoezi ambao tulikuwa tunafanya mazoezi ni tofauti bila shaka na ambao leo hii wanafanya.


"Hata kwenye uendeshaji unaona kabisa kuna mabadiliko kwa sasa, unajua zamani pale kila mtu alikuwa anaongea ila kwa sasa kuna uongozi ambao wapo watu wa kuzungumza," anasema kocha huyo raia wa Uholanzi.


Pluijm anasema: "Baadhi ya viongozi wanaongea sana halafu mazoezini hawaji, mimi nilikuwa na misimamo yangu kwa sababu najua mashabiki wanaipenda timu yao hivyo walikuwa wanahitaji matokeo mazuri tu na sio kitu kingine."


Amtaja Msuva


Kocha huyu aliopoulizwa kuhusu mchezaji ambaye anamkumbuka alipitia magumu na aliweza kumtengeneza kisaikolojia, anainama kidogo kisha na kumtaja Saimon Msuva.


Anasema Msuva alipitia wakati mgumu kiasi cha mashabiki kumkataa kila alipokuwa uwanjani, lakini aliendelea kumpa nafasi ili awanyamazishe na leo ni mmoja wa wachezaji tegemeo wa timu ya Taifa ya Tanzania.


"Msuva walikuwa wanamsema sana, lakini mimi nilikuwa namwambia utacheza na unachotakiwa kufanya ni kuwaonyesha kwamba unaweza kwa kuonyesha kipaji chako.


"Leo nenda kamuangalie Msuva yupo vipi, kama ningemkatisha tamaa kwa kipindi kile kwa kuamua kusikiliza nini baadhi ya watu na mashabiki wa Yanga wanataka basi ningempoteza," anasema.


Msuva pia aliwahi kukiri kupitia wakati mgumu kiasi cha mashabiki kutomuelewa, lakini aliendelea kupambana kuhakikisha anacheza kwenye kikosi cha Yanga kwa wakati huo.


Ashangaa kutimuliwa Azam FC


Pluijm baada ya kuondoka Yanga (2016) alienda Singid Utd kwa wakati huo lakini alikaa kwa mwaka miaka miwili (2017/2018) baada ya hapo alitimkia Azam FC ambapo alikaa (2018/2019).


Kocha huyo anasema akiwa na Azam alishangazwa kutimuliwa kwani sehemu ya mafanikio ni kuibadilisha timu hiyo kiuchezaji lakini pia kuchukua kombe la Mapinduzi.


 "Sawa kocha anaajiliwa ili afukuzwe kwahiyo sikushangaa kuondolewa lakini nakumbuka nilikuwa nimechukua ubingwa wa Mapinduzi, nazani kuna muda viongozi wawe wanaangalia timu nini inafanya;


"Ilinishangaza sana kwa sababu niliibadilisha timu kwa kiwango kikubwa sana kwenye upande wa uchezaji, kila mmoja aliona Azam ilivyokuwa inacheza nilipokuwa nayo."


Simu moja tu arudi Bongo


Baada ya kuondolewa AzamFC, Pluijm anasema alimalizana kila kitu na mabosi wa timu hiyo na kuondoka nchini na kwenda Ghana ambapo anaishi akiendelea na maisha yake mengine.


Msimu huu anasema amerejea baada ya kupigiwa simu na kigogo wa Singida Big Stars na kumwambia nini ambacho anatakiwa kukifanya katika timu hiyo kwenye Ligi Kuu.


"Bosi alinipigia simu na kuniambia kwamba amepata timu ambayo kwa sasa ipo Ligi Kuu, aliniambia tayari kuna kocha msaidizi Lule (Mathias), kwahiyo mimi nilipokuja nilimpa mipango yangu na tukashirikishana vizuri hadi sasa tunafanya vizuri," anasema.


Akuta wachezaji, amtaja Kaseke


Pluijm anasema hadi anakuja nchini tayari sehemu kubwa ya usajili kwa ajili ya msimu huu ulikuwa umeshafanywa, hivyo alichofanya ni kuingiza falsafa yake.


Kocha huyo anasema falsafa yake haikuwa rahisi kuigwa na wachezaji wake, lakini kidogo kidogo ilianza kuwaingia na ndiyo maana hadi sasa wanafanya vizuri kwenye mashindano wanayoshiriki.


"Nilikuja hapa nikiwa nimekuta wachezaji wamesajiliwa tayari na tulijitahidi kama benchi la ufundi kuweza kuwafanya waingie kwenye mifumo yetu na ndio maana tunafanya vizuri," anasema kocha huyo mwenye miaka 74.


Akizungumzia kuhusu kuendelea kumpa nafasi kiraka Deus Kaseke alisema hilo linatokana na namna ambavyo mchezaji huyo anavyoweza kuelewa kwa haraka kile ambacho anamuelekeza.


"Kaseke ana nidhamu sana na anapokuwa uwanjani anajituma kwahiyo ndio siri kubwa ambayo inanifanya nipende kufanya nae kazi kwa sababu nikimtuma kitu ndio anachoenda kukifanya.


"Nidhamu ndio kila kitu kwangu, mchezaji akiwa na nidhamu anakuwa bora kwa sababu atafata tu kile ambacho unamuelekeza," anasema Pluijm.


Nyota wa CAF kushushwa Singida BS


Singida imeshapata uhakika wa kucheza mashindano ya kimataifa, kocha Pluijm anasema hiyo ni fursa nzuri kwake kwani anataka kukisuka zaidi kikosi chake.


Anasema wachezaji ambao walisajiliwa msimu huu watakuwa ni mara mbili zaidi ya msimu ujao kwa sababu anataka kufanya makubwa kwenye mashindano ya Caf.


"Nataka nisajili wachezaji wenye viwango vya Caf kwa sababu hawa najua kabisa wakija hapa wataongeza ushindani kwa waliopo na itasaidia kufanya vizuri kwenye mashindano yote. Sitaki kushiriki tu, nataka nifike hatua ya makundi," anasema.


Kanu aanza kumkosha


Kwenye kikosi cha Singida Big Stars katika eneo la beki wa kati kwa sasa kuna kombinesheni nzuri kati ya Pascal Wawa na Biemes Kanu, hali inayowafanya washambuliaji wa timu pinzani kupata tabu kuwapita.


Pluijm anafichua kwamba beki huyo mwanzoni hakuwa sawa lakini alikuwa anatumia muda mwingi sana kumtengeneza kisaikolojia na kuendelea kumpa nafasi ya kucheza ili awe bora.


"Wakati anaanza Kanu hakuwa hivi ambavyo sasa anacheza, wengi walimuona kama beki wa kawaida, lakini niliona ana kitu ambacho anaweza kusaidia timu na niliendelea kumuamini," anasema.


Azigwaya Coastal, Mbeya City


Kocha huyu anasema mechi ngumu kwake alizokutana nazo ni dhidi ya Coastal Union, Mbeya City na ile dhidi ya Mtibwa Sugar, kwani kulikuwa na matukio mengi ndani ya dakika 90.


"Kiukweli mechi zangu mimi ngumu msimu huu ni za ugenini dhidi ya Coastal Union, Mbeya City na Mtibwa Sugar, hadi upate matokeo kwenye viwanja vyao vya nyumbani asee inabidi upambane kwa sababu kuna mambo mengi."


Katika kikosi cha Singida Big Stars yupo mchezaji Ibrahim Ajib, ambaye ameshacheza timu tatu kubwa nchini, ambazo ni Simba, Yanga, Azam FC na sasa yupo chini ya Pluijm.


Akiwa kwenye kikosi hicho bado hajawa mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha kwanza tofauti na ilivyo kwa mwenzake Said Ndemla ambaye ana uhakika wa kucheza.


Pluijm anamzungumzia kwa kusema tayari ameshakaa naye chini na kuzungumza na anachotakiwa kukifanya ni kuwaonyesha tu mashabiki kwamba bado anaweza.



Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz