Miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar (Historia ya Zanzibar) - EDUSPORTSTZ

Latest

Miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar (Historia ya Zanzibar)

Miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar

Miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar (Historia ya Zanzibar)

Miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar

Miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar

Leo ni maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo kwa mwaka huu hakutakuwa na gwaride kama ilivyozoeleka na fedha zilizotengwa kwa shughuli hiyo, zimeelekezwa katika miradi mbalimbali ya sekta ya Elimu Zanzibar.

Mapinduzi ya Zanzibar yalitokea mwaka 1964 ili kumuondoa madarakani Sultani wa Zanzibar na serikali yake, iliyoundwa hasa na Waarabu, na hatimaye kuweka uongozi mikononi mwa Waafrika, ambao ndio wengi visiwani humo (230,000 hivi), kwenye bahari ya Hindi, karibu na pwani ya Tanganyika.

Usultani wa Zanzibar ulikuwa umepewa na Uingereza uhuru wake mwaka 1963. Kabla ya hapo, Waarabu walikuwa wamefaulu kudumisha katika mfululizo wa chaguzi utawala waliokuwa nao tangu zamani za Zanzibar kuwa chini ya Usultani wa Omani.

Chama cha Afro-Shirazi Party (ASP), kilichowakilisha hasa Waafrika, kilipoona kwamba bungeni kina viti vichache ingawa kilipata 54% za kura katika uchaguzi wa Julai 1963, kilipatana na chama cha mrengo wa kushoto Umma Party.

Tarehe 12 Januari 1964 asubuhi na mapema, mwanachama wa ASP John Okello (1937-1971 ?) kutoka Uganda aliongoza wanamapinduzi 600–800 wa kisiwa kikuu cha Unguja kushinda polisi wa nchi na kuteka silaha zao.

Halafu walielekea Zanzibar Town walipompindua Sultani Jamshid bin Abdullah na serikali yake. Waliokufa katika mapigano wamekadiriwa kuwa 80 hivi.

Kumbe yalifuata kwa siku kadhaa (labda hadi tarehe 20 Januari) maangamizi ya kimbari dhidi ya wakazi wenye asili ya Kiarabu (waliokuwa 50,000 hivi) na ya Asia Kusini (waliokuwa 20,000 hivi); hakuna hakika kuhusu idadi ya waliouawa: makadirio yanataja kuanzia mia kadhaa hadi 20,000.

Kiongozi wa ASP Abeid Karume, asiyekuwa na msimamo mkali akawa rais wa kwanza wa nchi, na wanachama wa Umma party walipewa nafasi serikalini.

Kufikia Machi Okello alikuwa ameshawekwa pembeni na kufikia Aprili kikosi chake kimeshanyang’anywa silaha.

Mwelekeo wa Kikomunisti wa baadhi katika serikali mpya uliogopesha nchi za Magharibi. Kwa kuwa Zanzibar ilikuwa chini ya athari ya Uingereza, serikali yake iliandaa mipango kadhaa.

Hata hivyo, hofu ya kuundwa serikali ya Kikomunisti haikutimia kamwe, na kwa kuwa wananchi wa Uingereza na Marekani waliweza kuhama bila shida, mipango hiyo haikutekelezwa.

Wakati huo nchi za Kikomunisti za China, Ujerumani Mashariki na Umoja wa Kisovyeti zilianzisha mahusiano ya kirafiki na serikali mpya ya Zanzibar kwa kuitambua rasmi na kwa kutuma washauri.

Karume alifanikisha majadiliano ya kuunganisha Zanzibar na Tanganyika ili kuunda hatimaye muungano wa Tanzania; vyombo vya habari vilitafsiri muungano huo kuwa juhudi za kuzuia Ukomunisti kugeuza Zanzibar.

Mapinduzi yalikomesha miaka 200 ya utawala wa Waarabu Zanzibar, na yanaadhimishwa kila mwaka kama sikukuu ya taifa zima la Tanzania.

Historia ya Zanzibar inahusu historia ya eneo ambalo leo linaunda Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

HISTORIA YA AWALI

Mabaki ya vifaa vya mawe inaonyesha kwamba kwa kiasi cha miaka 20,000 kumekuwepo makazi ya binadamu katika visiwa vya Zanzibar.

Visiwa hivyo ni sehemu ya kumbukumbu ya kihistoria ya ulimwengu wakati Waajemi wafanyabiashara walivigundua na kuvifanya ndiyo makao makuu kwa safari kati ya Mashariki ya Kati, India na Afrika.

Katika karne ya mwanzo BK Zanzibar pamoja na mwambao wa Afrika ya Mashariki vilikuwa katika ufalme wa Saba.

Katika kipindi cha karne ya 3 na ya 4, Wabantu walianza biashara na Waarabu waliokuja Afrika ya Mashariki.

Katika karne ya 7, Waarabu walikuja Zanzibar kibiashara pamoja na kusambaza dini ya Uislamu, Waarabu ndio waliyoipa jina ZANZIBAR kutokana na maneno ya Kiajemi ZINJI BAR yaani sehemu ya Watu Weusi.

Lugha ya Kiswahili imeanza kutumika kiasi cha karne ya 13 ikitokana na mchanganyiko wa lugha ya Kiarabu na lugha za Kiafrika.

Katika karne ya 16 Wareno walikuja Zanzibar lakini utawala wao ulifuatiwa na kutokuwepo utulivu, lakini biashara ya utumwa iliwaweka watu pamoja.

CHINI YA WAARABU
Waarabu kutoka Oman walichukua utawala Zanzibar katika karne ya 17 na Zanzibar ilikuwa makao makuu ya utawala wa Waomani.

Miaka 1820-1870 Zanzibar ilifaidi matunda mazuri ya kiuchumi na maendeleo yaliyosababishwa na utawala wa kisultani na hivyo kupelekea Zanzibar kuwa na mwakilishi nchini Marekani na kupelekea kuenea kwa Dini ya Kiislamu.

Katika karne ya 19 Zanzibar ilikuwa chini ya utawala wa Oman, mwaka 1830 Zanzibar ilikuwa inaongoza kwa kilimo cha karafuu, na hiyo kupelekea haja ya watumwa kuongezeka kutumika katika kilimo. Hatimaye watumwa walikuwa 90% za wakazi wote.

SAYYID SAID KUHAMIA UNGUJA
Usultani wa Zanzibar ulianzishwa mwaka 1856 wakati Sultani Sayyid Said alipoamua kuhamisha makao makuu yake kutoka Maskat (Omani) kwenda Unguja.

Sayyid Said alikuwa Sultani wa Omani tangu mwaka 1804. Aliimarisha utawala wa Omani juu ya pwani ya Afrika ya Mashariki.

Mwaka 1829 alifaulu kuteka Mombasa iliyokuwa mji pekee wa kujitegemea kati ya miji yote ya Uswahilini.

Visiwa vya Unguja na Pemba vilikuwa chini ya Omani tangu mwaka 1689, Wareno walipofukuzwa katika pwani za Uswahilini.

BIASHARA YA KARAFUU NA WATUMWA
Sayyid Said aliona nafasi kubwa ya biashara ya karafuu kwa ajili ya soko la Uhindi na kwingineko. Mwaka 1829 akaanzisha mashamba ya mikarafuu kwa kutumia kazi ya watumwa kutoka bara.

Biashara hiyo ikabadilisha uso wa mji wa Zanzibar wa karne ya 19 uliowahi kuwa kijiji kikubwa tu cha vibanda kando ya boma lililojengwa na Omani kama kizuizi dhidi ya Wareno.

Baada ya azimio la mwaka 1832 la kuhamisha mji mkuu wa Omani kwenda Unguja, idadi ya wakazi wa mji ilikua haraka.

Nchi za nje zikatambua mji mkuu mpya na kujenga uhusiano. Ubalozi wa Marekani ulijengwa mwaka 1837, Uingereza ukafuata mwaka 1841 na Ufaransa mwaka 1844.

Sultani mwenyewe aliondoka kabisa Maskat mwaka 1840. Kukua kwa Zanzibar kulisababisha kukonda kwa mji wa Maskat

KUGAWIWA KWA OMANI KULIKUWA MWANZO WA ZANZIBAR
Baada ya kifo cha Sayyid Sultan mwaka 1856, usultani wa Oman uligawiwa kati ya wanawe. Sayyid Majid bin Said Al-Busaid (1834/1835–1870) akawa Sultani wa kwanza wa Zanzibar na kaka yake Sayyid Thuwaini bin Said al-Said akawa Sultani wa Oman akitawala nchi hiyo bila maeneo ya Afrika ya Mashariki.

Usultani mpya ulikuwa nchi yenye nguvu kati ya Rasi Delgado (mpakani na koloni la Kireno ya Msumbiji) hadi Mogadishu (Somalia). Athira yake ilienea kupitia njia za misafara ya pembe za ndovu na watumwa hadi mto Kongo.

Wafanyabiashara kama Tippu Tip waliokuwa raia wa Usultani wakapita Tabora na Ujiji kwenda ziwa Tanganyika na kuingia ndani ya eneo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya leo. Wapagazi wao walibeba bidhaa kutoka Zanzibar zilizobadilishwa kwa pembe za ndovu hasa. Watumwa walikamatwa au kununuliwa wakabeba pembe hadi pwani.

Pamoja na hayo, sultani alipokea kwa moyo wamisionari Wakristo.

Mapadri Wakatoliki wa kwanza pamoja na masista walitokea Reunion wakakaa Unguja tangu tarehe 12 Desemba 1860 hadi mwaka 1863, walipokabidhi misheni kwa shirika la mapadri wa Roho Mtakatifu.

Waanglikana wa chama cha Misheni ya Vyuo Vikuu kwa Afrika ya Kati U.M.C.A. (Universities` Mission to Central Africa) ambacho kiliundwa ili kutekeleza wito kutoka David Livingstone kuhubiri Injili na kukomesha utumwa katika Afrika, waliingia Zanzibar mwaka 1864.

Baadaye wakajenga kanisa kuu mahali pa soko la watumwa lililofungwa, altari ikiwa imejengwa juu ya nafasi ya mti wa kuwafunga watumwa walioadhibiwa kwa viboko, na batizio kuwa mahali walipotupwa watoto watumwa ambao hawakuuzwa pamoja na mama zao.

SAYYID BARGASH
Sultani wa pili wa Zanzibar yenyewe, Sayyid Bargash, alijitahidi kujenga uhusiano na nchi za nje. Alifunga soko la watumwa Zanzibar mjini kulingana na mapatano ya kimataifa, lakini akavumilia biashara ya watumwa kuendelea chinichini. Wakati wa Bargash majengo mengi ya Mji Mkongwe yakajengwa.

Mwishowe mwa utawala wake aliona kupungukiwa kwa eneo lake kutokana na mashindano ya nchi za Ulaya ya kuenea katika Afrika baada ya mkutano wa Berlin.

Mwaka 1885 Karl Peters alifanya mikataba ya ulinzi na watawala wadogo waliokuwa chini ya Sultani barani Tanganyika. Upingamizi wa Sultani ulishindikana kwa sababu Wajerumani walituma manowari Unguja akapaswa kukubali maeneo mapya ya Wajerumani.

KUENEA KWA UKOLONI
Mwaka 1886 mkataba kati ya Uingereza na Ujerumani ulibana eneo la sultani barani katika kanda yenye upana wa maili kumi tu kati ya Rasi Delgado na Mogadishu. Bargash na mfuasi wake Khalifa bin Said waliamua kuuza maeneo hayo au kuyakodisha.

1887/1888 pwani ya Kenya ilikodishwa kwa Waingereza. Wakati wa uhuru wa Kenya sehemu hii ikaingizwa katika Jamhuri ya Kenya.

Pwani ya Tanganyika ikakodishwa kwa Wajerumani mwaka 1888 na hatimaye kuuzwa mwaka 1890.

Miji kwenye pwani ya Somalia ikakodishwa kwa Italia mwaka 1892 ikauzwa mwaka 1906, ila Mogadishu mwaka 1924.

Hali halisi usultani ukabaki na visiwa viwili vya Unguja na Pemba tu.

Waingereza walikuwa walisita kuhusu Zanzibar lakini baada ya jaribio la Karl Peters la kufanya mkataba na Sultani ili kuingiza visiwa hivyo katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, Uingereza uliamua kutafuta utawala wa visiwa.

MKATABA WA ZANZIBAR-HELIGOLAND NA MWISHO WA UHURU

Mkataba wa Zanzibar-Helgoland kati ya Ujerumani na Uingereza ulileta patano la kuwa Zanzibar itakuwa chini ya Uingereza.

Tangu mwaka 1890 waziri mkuu wa Sultani alikuwa Mwingereza aliyepokea amri kutoka London.

Tangu mwaka 1913 nafasi ilichukuliwa na afisa mkazi mkuu.

Kwa muda wa miaka 26 usultani ulikuwa na fedha yake ya pekee iliyoitwa Riali ya Zanzibar.

Tangu mwaka 1890 Zanzibar ilikuwa chini ya uangalizi wa Waingereza rasmi, lakini uchaguzi wa mwanzo ulifanyika mwaka 1957, na miaka iliyofuata kukawepo fujo na machafuko kutoka kwa Waafrika wanaodai uhuru dhidi ya utawala wa Kiarabu.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokea tarehe 26 Aprili 1964 ukawa mwanzo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hadi tarehe ile kulikuwa na mataifa mawili huru ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambayo yaliingia mkataba wa muungano mnamo mwaka 1964 na kuanzishwa dola la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

MKATABA WA MUUNGANO

Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, tarehe 22 Aprili 1964 huko Zanzibar.

RAMANI YA ZAMANI

RAMANI YA ZAMANI

Mkataba huo ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi tarehe 26 Aprili 1964

Tarehe 27 Aprili 1964, viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na kubadilishana Hati za Muungano.

MABADILIKO YA JINA

Jina la “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar” lilibadilishwa baadaye, tarehe 28 Oktoba 1964, na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Sheria ya Jamhuri ya Muungano, Sheria namba 61 ya mwaka 1964.

MUUNDO WA MUUNGANO
Muundo wa Muungano wa Tanzania kama ulivyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, una vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji ambavyo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki ambavyo ni Mahakama ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Zanzibar; na vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma ambavyo ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashughulikia mambo yote ya Muungano kama yalivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara. Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inashughulikia mambo yote yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Visiwani.

SABABU YA MUUNGANO

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwepo kutokana na sababu mbalimbali kama vile kuwepo kwa mahusiano ya karibu na ya kihistoria baina ya Tanganyika na Zanzibar katika nyanja mbalimbali kama vile undugu wa damu, biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu kisiasa hususan baina ya vyama vya TANU na ASP.

Pia, azma ya kuwa na Muungano wa Afrika, hususan kwa kuanzia na Shirikisho la Afrika Mashariki. Hata kabla ya uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere pamoja na viongozi wengine waliokuwa wakipigania uhuru katika ukanda wa Afrika walikuwa na matarajio ya kuwa na Muungano wa Afrika. Mwalimu Nyerere binafsi alipendelea uwepo Muungano wa Afrika kwa kuanzia na Mashirikisho ya kikanda.

Kimsingi zipo sababu mbalimbali zilizosababisha Muungano huu kama vile historia za nchi hizo mbili, ukaribu wa nchi hizi mbili, muingiliano wa kijamii, ushirikiano wa kibiashara, ushirikiano madhubuti na wa muda mrefu wa kisiasa baina ya TANU na ASP, ushirikiano na urafiki wa muda mrefu kati ya watu, viongozi, na wakati wa harakati za utaifa uliopelekea uhuru wa nchi hizo mbili.

HATI ZA MAKUBALIANO YA MUUNGANO

Msingi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ni Hati za Muungano za mwaka 1964. Hati za Muungano zilitiwa saini na waasisi wa Muungano tarehe 22 Aprili 1964, na kupelekea Tanganyika na Zanzibar kuwa dola moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Baada ya Muungano, Mwalimu J. K. Nyerere alikuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya ya Muungano wa Tanzania na Sheikh Abeid Amani Karume, alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aprili 26, 1964 Bunge la Tanganyika lilipitisha Sheria za Muungano. Halikadhalika, Sheria hizo zilithibitishwa na Baraza la Mapinduzi Zanzibar. Sheria hizo za Muungano zilithibitisha Hati za Muungano, zilitaja Rais na Makamu wa Rais, zilitaja Muundo wa Muungano na Katiba ya Muungano.

MABADILISHANO ZA HATI BAINA ZA WAASISI

Aidha, Aprili 27, 1964, waasisi wa Muungano walibadilishana Hati za Muungano na wajumbe saba wa Baraza la Mapinduzi waliapishwa kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni Sheikh Abeid Amani Karume, Kassim Abdala Hanga, Abdulrahaman Mohamed Babu, Hassan Nassor Moyo, Sheikh Aboud Jumbe, Hasnu Makame na Sheikh Idris Abdul Wakil. Baada ya kuapishwa kuwa wabunge wakateuliwa kuwa mawaziri wa Serikali ya Muungano.

KABLA YA MUUNGANO

Kabla ya Muungano, kulikuwa na Katiba ya Tanganyika ya mwaka 1962 na upande wa Zanzibar kulikuwa na Amri za Katiba (Decrees). Katiba ya Tanganyika baada ya kufanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji ya Muungano iliendelea kutumika kama Katiba ya Muungano ya mpito hadi mwaka 1977 ilipopitishwa Katiba ya Muungano kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria za Muungano.

Aidha, marekebisho hayo yalimtaja Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, akiwa msaidizi wa Rais kwa masuala yote ya kiutawala kwa upande wa Zanzibar, na Waziri Mkuu kuwa ni Makamu wa Pili wa Rais ambaye atamsaidia Rais kwa masuala yahusuyo upande wa Tanganyika na kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni.

Katiba ya muda ya mwaka 1965 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliainisha mambo kumi na moja ambayo yalikubalika kuwa ni ya Muungano chini ya usimamizi wa Serikali ya Muungano ambayo ni pamoja na Katiba na Serikali ya Muungano. Mambo hayo ni: Mambo ya Nchi za Nje; Ulinzi; Polisi; Mamlaka juu ya mambo yanohusika na hali ya hatari; Uraia; Uhamiaji; Mikopo na Biashara ya Nchi za Nje na Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Mambo mengine ni Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania unaosimamiwa na Idara ya Forodha; na Bandari, mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu.

KUONGEZEKA KWA ORODHA YA MAMBO YA MUUNGANO

Mambo ya Muungano yaliongezwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria na kwa kushirikisha pande zote mbili za Muungano. Juni 10, 1965, mambo yote yahusuyo sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yoyote halali (pamoja na noti); benki (pamoja na zile za kuweka akiba) na shughuli zote za kibenki; fedha za kigeni na usimamizi wa mambo yanayohusu fedha za kigeni yaliingizwa kuwa jambo la 12 la Muungano.

Lengo kubwa la kuongezwa kwa jambo hilo lilikuwa kuwa na sarafu ya pamoja ya Tanzania baada ya Muungano, na kurahisisha usimamizi wa fedha za kigeni na benki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki mwaka 1964.

BAADA YA KUVUNJIKA KWA BODI YA SARAFU YA AFRIKA MASHARIKI 1964

Baada ya kuvunjika kwa Bodi hiyo, kila nchi mwanachama wa Jumuiya ililazimika kuwa na sarafu na mipango yake ya kusimamia mambo ya kibenki na fedha. Kufuatia kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1967, tarehe 11 Agosti 1967 mambo mawili yaliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano ambayo ni leseni za viwanda na takwimu (Jambo la 13), na elimu ya juu (Jambo la 14).

Mwaka 1968, suala la maliasili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta ya aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa na gesi asilia liliongezwa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano kuwa Jambo la 15.

KUVUNJIKA KWA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Vilevile, kufuatia kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977 na kutungwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, mambo yafuatayo yaliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano ambayo ni Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania na mambo yanayohusika na kazi za Baraza hilo (Jambo la 16); Usafiri; Usafirishaji wa Anga (Jambo la 17) na Utafiti (Jambo la 18); Utabiri wa Hali ya Hewa (Jambo la 19); na Takwimu (Jambo la 20).

Kutokana na kuvunjika kwa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki mwaka 1979, suala la Mahakama ya Rufani ya Tanzania nalo liliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa Jambo la 21. Vilevile, kufuatia mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Nyalali iliyokusanya maoni ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa, Uandikishaji wa Vyama vya Siasa na mambo mengine yanayohusiana nayo, liliongezwa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano (Jambo la 22). Suala hilo hatimaye lilipitishwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura Namba 258.

Utaratibu uliotumika katika kuongeza idadi ya Mambo ya Muungano kutoka 11 hadi kufikia 22 ni kupitia maamuzi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

HITIMISHO

Muungano umechukua nafasi kubwa katika kuwaunganisha wananchi na kuimarisha mahusiano mazuri baina ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka wigo mpana kwa wananchi wake kuweza kuzitumia fursa mbalimbali zilizopo za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa lengo la kujipatia maendeleo.

Nijuze TV ni App ambayo ukiwa nayo utaweza kutazama mechi za Ligi Kuu Tz Bara (NBC PREMIER LEAGUE) EPL, WORLD CUP, EPL, LALIGA, SERIA, LIGUE 1, BUNDESLIGA na Ligi nyingine nyingi.

DONWLOAD NIJUZE TV HAPA SISI kwetu Michezo ndiyo Furaha YETU.

Nipashe Michezo, Nijuze Michezo, Simba sc leo, Global Publishers michezo, saleh jembe michezo, Yanga leo, Shaffih dauda michezo, michezo, Magazeti, Usajili, Habari za Michezo, Nijuze Habari, Nijuze Michezo, Nijuze TV App, Nijuze TV LIVE, Nijuze Habari Michezo, Nijuze Habari Magazeti, Nijuze Habari Ajira, Nijuze Habari Usajili, Nijuze Habari Matokeo, Nijuze Habari Usajili, saleh jembe michezo leo,habari za michezo
leo 2023, habari za yanga za leo, habari za simba za leo, Habari za Michezo leo 2023.

The post Miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar (Historia ya Zanzibar) appeared first on Nijuze Mpya.



Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz