SIMBA Queens Mabingwa CECAFA 2022, Rais Samia awapongeza
Timu ya Simba Queens imetawazwa Mabingwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati CECAFA (SAMIA CUP 2022) baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya SHE Corporates ya Uganda, Mchezo wa Fainali uliofanyika kwenye wa Uwanja wa Azam Complex.
Mchezo ulikuwa mkali na wa kuvutia kutokana na timu zote kufahamiana vizuri kwani zilishakutana katika hatua ya makundi na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Mlinda mlango wa SHE Corporates alionyesha kiwango bora katika mchezo huo kwa kuokoa michomo ya washambuliaji wa Simba ambapo kama si ubora wake basi Mabingwa hao wa Uganda wangefungwa mabao zaidi ya moja walilofungwa.
Kiungo mkabaji Vivian Corazone ndiye aliyeipatia Simba Qeeens bao pekee la ushindi kwa mkwaju wa penati dakika ya 47 ambalo liliihakikishia Simba kubakisha taji hilo katika ardhi ya nyumbani.
Ubingwa huu unaifanya Simba kupata tiketi ya kuuwakilisha Ukanda wa CECAFA katika Ligi ya Mabingwa Afrika na inakuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kufanya hivyo.
Baada ya kutwaa Ubingwa huo wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan aliipongeza timu ya Simba Queens.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Rais Samia alituma salamu za pongezi na kuitakia heri katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake itakayofanyika nchini Morocco.
“Nawapongeza wanangu wa Simba Queens kwa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa Wanawake (SAMIA CUP). Mmejenga heshima kwa soka la Tanzania na nchi kwa ujumla.
“Nawatakia kheri katika Ligi ya Mabingwa Afrika (2022 CAF Women’s Champions League) itakayofanyika nchini Morocco,” ameandika Rais Samia.
Mchezaji wa Simba Queens, Aquino Corazone ndiye aliyeibuka mchezaji Bora wa Michuano ya CECAFA 2022.
Golikipa Simba Queens Gelwa Yona, ndiye Golikipa Bora wa michuano ya CECAFA.
The post SIMBA Queens Mabingwa CECAFA 2022, Rais Samia awapongeza appeared first on Nijuze Mpya -| Pata Habari zote za Michezo kitaifa na Kimataifa, Tetesi na Usajili, Magazeti ya Michezo, Ratiba na Matokeo, Mahusiano Pamoja na Nafasi za Kazi.
No comments:
Post a Comment