Simba Yamshangaa Bernad Morrison Kutoa Shutuma Kwa Viongozi Kupitia Vyombo vya Habari - EDUSPORTSTZ

Latest

Simba Yamshangaa Bernad Morrison Kutoa Shutuma Kwa Viongozi Kupitia Vyombo vya Habari



KLABU ya Simba imedai kushangazwa na Benard Morrison kutoa shutuma kwa viongozi kupitia vyombo vya habari badala ya kufuata taratibu zinazohusika kama anaona hakutendewa haki.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu amesema kuwa anamshangaa mchezaji huyo kudai alilazimishwa kwenda mapumziko ya lazima wakati hakuwa na matatizo ya kifamilia, lakini alishindwa kulalamika au kukataa wakati huo hadi kuibuka sasa, hivyo kuonesha huenda analishwa maneno.

Murtaza alisema hayo juzi, ikiwa ni siku moja baada ya mchezaji huyo ambaye anamaliza mkataba wake na klabu hiyo Agosti 14, kutoa maelezo kadhaa, ikiwemo shutuma kwa baadhi ya viongozi, akidai hata alipoandikiwa barua ikidai kuwa alikuwa na matatizo ya kifamilia, hivyo aende kwao akayatatue, haikuwa kweli kwamba alikuwa na matatizo.

Alisema hayo alipokuwa akihojiwa na chombo kimoja cha habari.

"Alisaini mkataba wa ajira na Simba kwa ridhaa yake, kama alikuwa hajaridhishwa na kitu chochote mbona hakusema au kufuata taratibu zilizopo kwa sababu kwenye mkataba kumeainishwa haki zake na za klabu, kwa nini hakufanya hivyo? Yeye ndiye aliyetaka ruhusa kwenda kutatua matatizo ya kifamilia, klabu ikampa, akakubali kwa nini leo amegeuka ghafla baada ya kurejea kutoka huko alikotoka? Na kama alikuwa hana la kufanya huko kwa nini alikwenda kwao?." Alihoji Mangungu.


Alisema Morrison bado ni mchezaji wa Simba na kuachwa au kubaki itategemea benchi la ufundi litakavyoamua.

Kuhusu kukataliwa barua ya kuondoka kwenye klabu hiyo, mwenyekiti huo alisema wapo wachezaji ambao wao na klabu zinazowataka zimeomba na wamepata, ila yeye ameamua kuomba kwa kupitia mitandao ya kijamii, kitu ambacho si utaratibu.

"Yeye ameamua kujadiliana kwenye vyombo vya habari badala ya kuiambia klabu inayomtaka kuomba barua rasmi, anaomba kupitia mitandao ya kijamii, basi aendelee," alisema.


Morrison, raia wa Ghana aliyejiunga na Simba misimu miwili iliyopita akitoka Yanga, anadaiwa kuwa na mpango wa kurejea kwenye klabu yake hiyo ya zamani.







Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz