TIMU ya Taifa ya Ukraine imefanikiwa kwenda Fainali ya mchujo wa kuwania tiketi ya Kombe la Dunia baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wenyeji, Scotland usiku wa jana Uwanja wa Hampden Park Jijini Glasgow.
Mabao ya Ukraine yamefungwa na
Andriy Yarmolenko dakika ya 33,
Roman Yaremchuk dakika ya 49 na Artem Dovbyk dakika ya 90 na ushei, wakati la Scotland limefungwa na Callum McGregor dakika ya 79.
Sasa Ukraine itakutana na Wales Jijini Cardiff Jumapili katika mechi ya kupata timu ya kushiriki Fainali za Qatar zinazotarajiwa kuanza mwezi Novemba na ataungana na timu za England, USA na Iran katika Kundi B.
Jana Ukraine wamecheza mechi ya kwanza ya mashindano tangu wavamiwe na majeshi ya Urusi mwezi February, ambayo ilisababisha mechi hiyo kuahirishwa kutoka Machi hadi June.
Kwa ujumla soka ilisimama kuchezwa Ukraine baada ya kuvamiwa na majeshi ya Russia, lakini kikosi cha wachezaji 21 wanaocheza nyumbani kutoka klabu za Shakhtar Donetsk na Dynamo Kyiv kiliweka kambi Slovenia tangu mwanzoni mwa Mei na kucheza mechi tatu za kirafiki dhidi ya klabu za Ujerumani, Italia na Croatia.
Na kuelekea mechi na Scotland kiliongezewa nguvu na wachezaji wanaocheza ligi nyingine za Ulaya ikiwemo LIgi Kuu ya England, Oleksandr Zinchenko, Vitaliy Mykolenko na Andriy Yarmolenko.
Awali timu hizo zilikutana mara mbili kwenye mechi za kufuzu Euro 2008 na kila moja ilishinda mara moja.
No comments:
Post a Comment