MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imeamua wabunge 19 wa CHADEMA waliovuliwa uanachama waendelee kuwapo bungeni hadi maombi ya zuio la muda yatakaposikilizwa Juni 13, mwaka huu na kutolewa uamuzi.
Wabunge wa kambi ya upinzani bungeni wakiwa kwenye kikao cha Bunge jijini Dodoma, jana. Licha ya kuvuliwa uanachama na chama chao bado wanahudhuria vikao hivyo kama kawaida. PICHA: IBRAHIM JOSEPH
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Mfawidhi John Mgeta wa Mahakama hiyo baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili.
Alisema hoja zilizowasilishwa ni nyingi na maombi yameletwa kwa hati ya dharura.
Pia alisema wabunge 19 wapo bungeni, waendelee kuwa bungeni hadi maombi yao yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Alisema wajibu maombi watatakiwa kuwasilisha viapo kinzani mahakamani hapo kujibu mambo yaliyowasilishwa na waleta maombi.
Awali Wakili wa Halima Mdee na wenzake, Aliko Mwamanenge, aliomba mahakama itoe zuio la muda ambalo litawafanya waleta maombi wote kuendelea kushikilia nafasi zao bungeni kama wabunge wa viti maalumu.
"Tunaomba amri hii iendelee hadi tutakaposikilizwa maombi yetu kwa pande zote mbili na kutolewa maamuzi," alidai Mwamanenge.
Mjibu maombi, Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata, alidai baada ya kutafakari tuhuma zilizotolewa na mjibu maombi namba mbili na tatu wanaiachia mahakama ione mazingira hayo kama yanawezesha Jaji kutoa amri hizo.
Pia aliomba wapatiwe muda na mahakama wa kupitia maombi yaliyowasilishwa ili waweze kujibu kiapo kinzani.
Mawakili wa CHADEMA, Peter Kibatala na Jeremia Mtobesya, waliwasilisha hoja sita za kupinga ombi la kutolewa kwa amri ya muda kutokana na upungufu katika maombi na viapo vya waleta maombi.
Akiwasilisha hoja hizo, Kibatala alidai kuwa katika hoja ya kwanza viapo vya waleta maombi sehemu moja wamesaini mawakili badala ya waleta maombi.
Alidai kuwa, pingamizi la pili hakuna kiapo kinachotaja dini zao, hamna kiapo kama dini, uhai wa kiapo ni maombi yenyewe.
Katika pingamizi la tatu, Kibatala alidai maombi yaliyowasilishwa hayajaonyesha kuwa yanataka nini na dhidi ya kina nani, amri ikitolewa itakuwa imetolewa dhidi ya nani na kwamba haitaeleweka.
“Amri za mahakama zinatakiwa ziwe zinaeleweka na kutekelezeka. Mheshimiwa Jaji haujaombwa, kwa hiyo hawawezi kutoa amri kwa sababu hakuna sehemu waliyokupeleka kufikia kutoa nafuu hizo," alidai Kibatala.
Pingamizi la nne, Kibatala anaeleza kuwa amri haiwezi kutolewa kwa sababu Bunge (Katibu wa Bunge) hayupo katika shauri hilo, wakati ofisi yao ndiyo inashughulikia masuala ya waleta maombi.
Kibatala anaendelea kuwasilisha mapingizi yake, kuwa katika pingamizi la tano Katiba inakataza suala lililofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuchunguzwa.
Katika pingamizi la sita, hakuna sababu zozote zilizotolewa kuonyesha kwamba kuna hatari itatokea kama waleta maombi wakitolewa bungeni, “kwa hiyo jaji hajapewa hoja za kuthibitisha hiyo hatari.”
Akijibu pingamizi hizo, Wakili Aliko aliiomba mahakama kutupilia hoja hizo na kuwapatia zuio la muda kama walivyoomba kwa sababu hoja walizotoa hazina mashiko.
Alidai, katika suala la viapo kutokuwa na dini sio suala la kisheria, kwa sababu mapingamizi yao sita kama walitaka kuyazungumzia walitakiwa kuwa na kiapo walichoapa kitakachokataa viapo vyao kuwa vina upungufu.
Halima Mdee na wenzake wamewasilisha maombi mawili Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ya kibali cha kufungua kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama na Baraza Kuu la CHADEMA, ambalo lilikaa Mei 12, 2022 na kufikia uamuzi huo baada ya kupigwa kura nyingi.
Maombi hayo yamefunguliwa dhidi ya bodi ya wadhamini ya CHADEMA, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Pia, wamefungua maombi ya zuio la muda (injunction) wakiomba waendelee kuwa wabunge hadi uamuzi wa maombi yao utakapotolewa.
No comments:
Post a Comment