Serikali Yataja Sababu za Kukatika Umeme - EDUSPORTSTZ

Latest

Serikali Yataja Sababu za Kukatika Umeme




Dodoma. Serikali imetaja sababu za kukatika kwa umeme mara kwa mara ambapo imesema mgandamizo mkubwa wa nishati hiyo unaotokana na mahitaji makubwa ya umeme ndio chanzo cha changamoto hiyo.

Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Felchesmi Mramba ameyasema hayo leo Jumanne Novemba 9, 2021 wakati akielezea mafanikio na maendeleo ya sekta ya nishati katika miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara.

Amesema katika miaka ya 2013 hadi 2015 walikuwa na miradi mingi ya kujenga vituo vya usambazaji umeme katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni Kipawa, Ilala Mbezi Beach na Makumbusho (mkoani Dar es Salaam), Arusha, Singida na Dodoma.


Pia amesema licha ya kujenga vituo vingi sana walijenga laini nyingi sana za usambazaji umeme.

Amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi huo kililipa nafuu kubwa lakini kadri miaka inavyoongezeka mahitaji ya umeme yanaongezeka na hivyo ahueni iliyopatikana haiwezi kuwa ahueni ya kudumu.

“Kwa hiyo ni lazima kazi nyingine ziendelee kwa ajili ya kuleta ahueni siku mbele. Mnafahamu tayari miradi mingine inaendelea ya kuimarisha umeme ambayo itatupa tena ahueni,”amesema.


Amesema kwa kawaida Oktoba na Novemba ukichora mchoro wa mahitaji ya umeme huwa yanapanda juu.

Amesema mahitaji ya umeme Novemba mwaka huu ya juu yalikuwa ni Megawati 1273, kiasi ambacho hakijawi kufikiwa katika historia Tanzania.

Amesema kuwa matumizi ya umeme yanavyoongezeka mfumo unakuwa mgandamizo mkubwa na hivyo kubeba umeme mwingi zaidi, jambo ambalo linasababisha waya kupata moto na hivyo uwezekano wa kukatika umeme kuwa mkubwa zaidi.

Hata hivyo amesema kuna miradi ya kuboresha mifumo kwa kujenga vituo na kuimarisha vituo unaendelea.


Amesema lililojitokeza hivi karibuni la kukatika kwa umeme ni tatizo la muda mfupi litadhibitiwa na halitaendelea kusumbua tena kwa kiwango kikubwa.




Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz