Machinga waanza kuondolewa barabarani - EDUSPORTSTZ

Latest

Machinga waanza kuondolewa barabarani




 
HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza,  imeanza kuwaondoa barabarani wafanyabiashara wadogo, maarufu kama machinga na kuwahamishia maeneo rasmi kama alivyoagiza Rais Samia Suluhu Hassan.

Wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga, wakiendelea na shughuli zao licha ya kuwepo bango lililowekwa na Manispaa ya Kinondoni la amri ya kutofanya biashara kwenye eneo la Mwenge, Barabara ya Bagamoyo, mkoani Dar es Salaam jana. PICHA: MIRAJI MSALA
Kwa kuanzia, manispaa hiyo imeanza kukagua miundombinu kwenye masoko yote, ili kuyarekebisha kabla ya kuanza kuwapanga machinga katika maeneo rasmi ya kufanyia biashara.

Hayo yalibainishwa jana  na Mkuu wa Wilaya hiyo, Hassan Masalla, baada ya kumaliza ziara yake ya kata zote 19 na kuitisha kikao cha majumuisho kilichowahusisha madiwani, wenyeviti wote wa mitaa, watendaji, walimu wakuu wa shue za msingi na sekondari .

Masalla alisema uongozi wa halmashauri hiyo, umeanza mchakato huku moja ya mikakati yao ni kutembelea maeneo yote ya masoko kujiridhisha kama kuna mahitaji muhimu ikiwamo maji na vyoo, ili kuweka mazingira bora kwa wafanyabiashara hao.

Alisema wananchi kufanya biashara holela ni tatizo  wilayani hapa, hivyo wakati umefika kupanga maeneo, ili biashara zifanyike kwa kufuata utaratibu.


 
Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa, maeneo muhimu watakayoyatembelea kukagua miundombinu ni pamoja na soko la Kiloleli, Nyasaka, Kirumba, Sabasaba na Buzuruga .

Alisema ana imani kuwa kazi hiyo itafanyika kwa utulivu , amani na ushirikiano na kwamba hawatatumia migambo wala polisi na kwamba halmashauri hiyo, itakuwa ya mwisho kutumia nguvu kwa kuwa wamezungumza na viongozi na mazungumzo yanaendelea ili kuona ni gani kero wanazokutana nazo, ili wasaidiane kuzitatua.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ilemela, Dk. Angeline Mabula, alisema awali kuwa kazi ya kuwapanga machinga kwenye maeneo yao ilienda vizuri na  walihamia kwenye maeneo husika.


Dk. Mabula alisema bado ana imani kwa sasa kazi hiyo itafanyika vizuri kwa kuwa wafanyabiashara hao ni waelewa na wakishirikishwa wataenda, bila manung’uniko yoyote.

“Kazi hii awali ilifanyika vizuri, lakini alitokea mtu mmoja akampigia simu Hayati Rais John Magufuli na kumweleza machinga wameteswa na wamevunjiwa vitu vyao ndipo akaagiza warudishwe kwenye maeneo waliyokuwapo, hivyo niombe viongozi wote tushirikiane kwa pamoja kuhakikisha kazi hiyo, inaenda vizuri na kuisha kwa amani,” alisema Mabula.




Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz