Askofu Gwajima njiapanda - EDUSPORTSTZ

Latest

Askofu Gwajima njiapanda



 
NI njiapanda! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na azimio la Bunge dhidi ya Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima.

Baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumtia hatiani kwa utovu wa nidhamu, jana Bunge lilipitisha azimio la kumfungia kushiriki mikutano miwili ya chombo hicho.

Bunge pia liliazimia vyombo vya dola vichukue hatua kutokana na kauli zilizotolewa na Gwajima na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichompa ridhaa ya kuwa mbunge, kimwajibishe kwa mujibu wa taratibu zake za ndani ya chama.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Emmanuel Mwakasaka, alitumia dakika 38 kuanzia saa 4:36 asubuhi kuwasilisha bungeni taarifa yao kuhusu shauri la Askofu Gwajima, akisisitiza mbunge huyo hakutoa ushirikiano kwa kamati.

Kwa mujibu wa Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, Gwajima alihojiwa na kamati kuhusu kauli zake alizozitoa Julai 25, 2021, Agosti Mosi, 2021 na Agosti 15, 2021 akiwa maeneo ya Ubungo mkoani Dar es Salaam.


 
Alisema mbunge huyo alifika mbele ya kamati kuhojiwa na alikiri kutoa kauli zinazolalamikiwa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, akisisitiza ni mahubiri yake kanisani na hayapaswi kuhojiwa bungeni.

Mwakasaka alisema kutokana na kauli hiyo ya Gwajima, kamati ililazimika kurejea Ibara 19 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 kuhusu uhuru wa kuabudu ambayo imeelekeza masuala ya kuabudu kuzingatia sheria za nchi ili kulinda maadili katika jamii.

"Kamati ilijiridhisha mahubiri yanayotolewa yanapaswa kulinda usalama na maadili kwa jamii na tuliporejea Ibara ya 30 ya Katiba hiyo, tulibaini hakuna kinga ya mahubiri ya kanisani kuhojiwa.


"Mheshimiwa Josephat Gwajima ni mbunge na askofu. Anapaswa kuwa mfano bora kwa jamii. Kamati imejiridhisha kuwa kauli za Mheshimiwa Gwajima zinadhalilisha Bunge na kuchonganisha mihimili. Kauli hizi ni utovu wa nidhamu uliokithiri," alisema.

Mwakasaka aliendelea kubainisha kuwa akiwa mbele ya kamati, Gwajima alionyesha kuwa mtu mwenye jeuri na kejeli kwa kamati na alishindwa kuthibitisha kauli zake na hakuwa na kielelezo chochote licha ya kuwaaminisha wananchi kwamba anao ushahidi kuhusu kilicho nyuma ya chanjo ya corona.

"Mheshimiwa Gwajima alishindwa kuthibitisha viongozi kupewa rushwa ili kuidhinisha chanjo ya corona aina ya Johnson & Johnson na hivyo kamati ilimtia hatiani.

"Shahidi Gwajima alipofika mbele ya kamati na kukataa kutumia kiti kilichoandaliwa, akakataa kutumia kipaza sauti na hata kufikia hatua ya kuhojiwa akiwa amesimama. Kamati iliamua kumvumilia.


 
"Gwajima hakutoa ushirikiano kwa kamati na kwenye maeneo mengi, hata yaliyohitaji majibu mafupi, alielezea masuala ya imani yake na kujivunia idadi kubwa ya waumini wake waliopo maeneo mbalimbali duniani," alisema.

Mwakasaka alisema kamati yao katika kufuatilia mwenendo wa shahidi huyo, ilibaini ni mkaidi na jeuri na hakutaka kujutia kauli zake licha ya kuwa zinachonganisha mihimili na kupotosha wananchi.

Kamati hiyo ilipendekeza Askofu Gwajima apewe adhabu hiyo ya kutoshiriki mikutano miwili ya Bunge na vyombo vingine vichunguze kauli zake zenye mwelekeo wa uchochezi na upotoshaji.

Pia ilipendekeza Gwajima achukuliwe hatua na chama kilichompa ridhaa ya kuwa mbunge, CCM. Bunge liliridhia azimio hilo.


Kutokana na kusimamishwa kushiriki shughuli za Bunge, Spika Ndugai alitangaza kuwa Gwajima na Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa (CCM), watakuwa wanalipwa nusu ya mishahara na posho zingine za kibunge kwa kipindi chote cha adhabu kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge




Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz