Uviko-19 wadaiwa kusababisha upungufu wa nguvu za kiume - EDUSPORTSTZ

Latest

Uviko-19 wadaiwa kusababisha upungufu wa nguvu za kiume


Madaktari wamebaini kuwa virusi vipya vya Uviko-19 vinaweza kusababisha upungufu wa nguvu za kiume.

Hata hivyo takwimu za mwisho zilizotolewa na Wizara ya Afya nchini Agosti 15, zilionyesha kuwa walengwa 207,391 wamepatiwa chanjo ya Uviko-19 mpaka kufikia Agosti 14 mwaka huu.

Takwimu hizo zinaonyesha wanaume wamechanjwa kwa asilimia 58.3 sawa na 121,002 huku wanawake waliochanjwa ni 86,389 sawa na asilimia 41.7.

Madaktari waliofanya utafiti huo kutoka Chuo Kikuu cha Miami nchini Marekani wameeleza kuwa athari hizo zinatokana na ukweli kwamba virusi hivyo vinaathiri zaidi mishipa ya damu hasa ile inayopeleka damu moja kwa moja kwenye uume.


 
Watafiti hao, wakitumia darubini maalumu ya kitabibu wamebaini kuwepo kwa virusi vya Uviko-19 kwenye vinasaba maalumu vilivyochukuliwa kwa wagonjwa wawili ambao wanadaiwa kupoteza nguvu za kiume baada ya kupata maambukizi, waliyoyapata kati ya miezi sita na  minane iliyopita.

Alipoulizwa kuhusu utafiti huo, Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Elisha Osati amesema kuna ukweli kuhusu utafiti kwani Uviko-19 unaathiri vijana.

“Sitaki kuwatisha watu lakini ukweli ni kwamba unaweza hata kupoteza nguvu na mbegu za kiume kwa kuwa na Uviko-19 na kushambulia mapafu, figo na mishipa ya damu inashambulia pia via vya uzazi kwa wanaume inaweza kuleta madhara na kuzuia utengenezwaji wa mbegu za kiume na kwa wanawake pia.


“Vijana wengi wasibweteke huu ugonjwa ukiupata unaweza kuwaletea madhara kwa namna moja ama nyingine hatutaki kuwa na watu ambao hawawezi kuzaa na kupata watoto au kujenga taifa waende kupata chanjo mimi nakaa na wagonjwa ICU na baadaye wanakuwa wanahudhuria kliniki mrejesho tunaupata matokeo yake si mazuri,” amesema Dk Osati ambaye pia ni mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya.

Daktari bingwa wa fiziolojia ya homoni na mazoezi kutoka Chuo Kikuu cha Afya Kishiriki cha Sayansi Muhimbili (MUHAS), Fredrick Mashili amesema kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya damu na nguvu za kiume.

“Ili nguvu za kiume zitokee damu inahusika na ndiyo kisababishi ndiyo maana mtu akiwa na shida katika mishipa ya damu au ugonjwa utakaoathiri mishipa ya damu lazima tatizo la upungufu wa nguvu za kiume hutokea,” amesema.

Amesema damu na ubongo vinahusika katika tendo hilo lakini kikubwa ni vichocheo ‘homoni ya kiume’ ambapo kiwango cha homoni hii huongezeka zaidi nyakati za asubuhi.


 
“Kwenye uume kuna mishipa mikubwa ya damu, halafu wenyewe upo kama sponji hivyo mwanaume anavyojengeka kisaikojia kuwa tayari kwa lile tendo damu hutoka katika maeneo mengine ya mwili na kushuka chini damu ikienda katika uume hushibisha ile mishipa inatanuka, uume hurefuka na kunenepa na ndipo nguvu za kiume hutokea,” amesema Dk Mashili.

Utafiti

Kwa mujibu wa jarida la World Journal of Men's Health la Marekani, tafiti zaidi zimebaini kuwa kuharibiwa kwa mishipa ya damu kwenye uume wa wagonjwa wa Uviko-19 imethibitishwa baada ya kufanya uwiano na wengine wawili ambao hawajaathiriwa na Uviko-19 ambao tayari walishapata tatizo hilo.

"Tulibaini kuwa virusi hivi viliathiri mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye uume, hivyo kusababisha uume kukosa nguvu," amesema Dk Ranjith Ramasamy, mtafiti mwandamizi ambaye pia ni Mkurugenzi wa mpango wa urology ‘mfumo wa mkojo wa mwanaume’ katika Chuo Kikuu cha Tiba Miami.

"Hii mishipa ya damu imebainika kuwa imeharibiwa na hivyo kuziba, kwa hiyo haiwezi kifikisha kiwango cha damu kinachohitajika kwa ajili ya kuupa nguvu uume," ameongeza.


Dk Ramasamy amefananisha athari hiyo na zile zinazovikumba viungo vingine ikiwemo mapafu, figo na ubongo, ambazo zimekuwa zikiwakabili wagonjwa wa Uviko-19.

"Tunadhani uume pia unaathirika kwa namna hiyo. Hatufikirii kwamba hili linaweza kuwa tatizo la muda mfupi, tunadhani linaweza kuwa tatizo la kudumu," amesema.

Ripoti mpya iliyolenga wagonjwa wawili wengine wa Uviko-19 ambao walifanyiwa upasuaji wa sehemu za siri ilibaini kuwa wote walikuwa na nguvu za kiume za kutosha kabla ya kupata maambukizi.

Mmoja kati yao aliugua Uviko-19 na kulazwa hospitali kwa wiki mbili kabla ya kupata nafuu, lakini hakuwa na magonjwa sugu.

Mwingine aliugua Uviko-19 lakini alikuwa na matatizo kwenye mishipa ya damu yanayotokana na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu, kabla ya kupata maambukizi hayo.


 
Wote wawili bado wanaonekana kuwa na vimelea vya Uviko-19 katika seli zao  na kwa sehemu wanaonekana kupata matatizo ya mishipa midogo ya damu kutofanya kazi ipasavyo, hivyo kushindwa kufikisha damu katika baadhi ya maeneo ya mwili.

Kwa uwiano, mmoja wa watu ambaye hajaugua corona lakini anafanyiwa tiba ya kupoteza nguvu za kiume, haonyeshi kuwa na tatizo la kuharibiwa mishipa midogo ya damu kama ilivyo kwa hao walioathiriwa na Uviko-19.

"Nadhani hili siyo suala ambalo wanaume wanalijadili kwa sasa kutokana na mambo yanavyokwenda. Lakini nina uhakika katika miezi sita ijayo, hadi mwaka mmoja mbele tutakuwa na jambo lenye ukweli kuhusu athari za Uviko-19 kwa wanaume ambao hawakuwa na tatizo la nguvu za kiume," amesema Ramasamy.

Kwa upande wake, mtaalamu wa mfumo wa mkojo kwa mwanaume ‘urology’ katika Chuo cha Tiba cha Icahn  Mount Sinai mjini New York, Dk Ash Tewari amesema inaingia akilini kwamba Uviko-19 inaweza kuwaathiri wanaume kwa namna hiyo, kutokana na uwezo wa virusi hivyo kuathiri mishipa ya damu.

Hata hivyo amehadharisha kuwa wanaume hawatakiwi kutaharuki hadi tafiti zaidi zitakapofanyika na kutoa matokeo yake.

"Mgonjwa mmoja au wawili hawawezi kuwa uthibitisho wa tatizo, lakini hii ni hatua inayochochea zaidi tafiti na uchunguzi. Athari za Uviko-19 ni kwamba inaathiri mishipa midogo ya moyo kama inavyoweza kuathiri mishipa midogo kwenye uume," amesema.

Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz