Chadema wahudhuria ibada kumuombea Mbowe, Katiba Mpya - EDUSPORTSTZ

Latest

Chadema wahudhuria ibada kumuombea Mbowe, Katiba MpyaMwanza. Viongozi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Ziwa wamehudhuria katika ibada maalum ya kumuombea mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe anayekabiliwa mashtaka ya uhujumu uchumi kwa kula njama na kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi.

Ibada hiyo ilifanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) lilipo Furahisha jijini Mwanza ambapo baadhi ya viongozi wa chama hicho Kanda ya Ziwa na wanachama waliohudhuria ibada hiyo walivaa sare za chama hicho.


 Akizungumza na Mwananchi baada ya ibada hiyo, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi amesema ibada hizo ni mkakati mpya wa kudai katiba mpya na kumuombea mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe.


Obadi amesema mkakati huo ni wa amani na unalenga kuongeza uelewa kwa wananchi kwamba suala la kudai katiba mpya siyo la Chadema peke yake bali wananchi wote.


“Tuna nia ya pamoja ya kumuombea mwenyekiti wetu wa taifa na tunamuombea Rais Samia Suluhu Hassan kwa Mungu akampe hekima katika hili jambo kwa sababu linahatarisha amani ya nchi, tunaamini kumshikilia kiongozi wetu wa taifa haileti afya kwa taifa,” amesema Obadi nje ya kanisa akiwa na baadhi ya viongozi wa kand hiyo na wanachama waliokuwa wamevaa sare za chama hicho.


Naye mwenezi wa Baraza la Vijana wa Chadema Taifa (Bavicha), Twaha Mwaipaya alisema ibada hizo zitasaidia kupunguza maumivu na mikikimikiki ambayo wamekuwa wakiipitia katika mchakato wa kudai katiba mpya nchini.


“Chadema tunapitishwa katika wakati mgumu sasahivi, tunaamini mwenyekiti wetu (Freeman Mbowe) siyo gaidi, yote anayopitia ni kwa sababu alisimama mstari wa mbele kwa ajili ya kuhesabiwa haki katika taifa lake ndiyo maana tumekuja kumkabidhi Mungu kilio chetu,” alisema Mwaipaya.
Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz