Ndugu Wauana Kisa Penzi la Mke wa Kaka Yao - EDUSPORTSTZ

Latest

Ndugu Wauana Kisa Penzi la Mke wa Kaka Yao

MWANAUME aliyejulikana kwa jina la Kiseri Ndaletyan (38) mkazi wa kitongoji cha Naamalasin kata ya Noondoto tarafa ya Kitumbeini Wilaya ya Longido Mkoa wa Arusha amefariki dunia baada ya kukatwa kitu chenye ncha kali shingoni na mdogo wake Melita Ndaletyan (34).

 

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justine Masejo tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana Julai 8,2021 majira ya saa sita na nusu katika kitongoji cha Naamalasin kata ya Noondoto tarafa ya Kitumbeini Wilaya ya Longido.

 

“Kiseri Ndayetyan (38) mfugaji mkazi wa kijiji cha Noondoto alifariki dunia baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na mdogo wake Melita Ndayetyan (34) mfugaji mkazi wa Noondoto.

 

Chanzo cha tukio hilo ni tamaa ya kimapenzi, baada ya mtuhumiwa Melita Ndayetyan kutaka kumuingilia kimwili mke wa kaka yake na kuzuiwa na marehemu kufanya jambo hilo,” amesema Kamanda Masejo.

 

Amesema mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi na mara baada ya upelelezi kukamilika jarada litapelekwa Ofisi ya mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.

 

Kamanda Masejo pia ametoa ufafanuzi kuhusu tukio la ukatili dhidi ya mtoto mdogo mwenye umri miaka minne (04) ambaye jina lake limehifadhiwa Mkazi wa Majengo jijini Arusha aliyekutwa ametelekezwa maeneo ya Burka kata ya Olasiti Tarafa ya Elerai katika jiji la Arusha.

 

“Tarehe 06/07/2021 muda wa 12:00 hrs huko maeneo ya Burka kata ya Olasiti Tarafa ya Elerai katika jiji la Arusha,Mtoto mdogo umri miaka minne (04) jina lake limehifadhiwa Mkazi wa Majengo jijini Arusha, alikutwa ametelekezwa maeneo ya Burka.

 

“Taarifa za awali zilibaini kwamba mtoto huyo alifanyiwa ukatili wa kipigo pamoja na kuwekewa majani mdomoni na baba yake wa kufikia. Jeshi la Polisi liliendelea na upelelezi na kubaini kwamba, kuna mgogoro wa kifamilia kati ya mama wa mtoto huyo na baba wa kufikia jina limehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi,” ameeleza.

 

Amesema mara baada ya kufanya tukio hilo mtuhumiwa alikimbia na Jeshi la Polisi mkoani Arusha lilifanya jitihada za kumtafuta kwa kushirikiana na raia wema na kufanikiwa kumkamata.

 

“Nitoe wito kwa wananchi kutoa taarifa dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa watoto kwa Jeshi la Polisi ili kukomesha au kumaliza kabisa tatizo la unyanyasaji kwa watoto. Pia niwaonye wenza wenye migogoro katika familia kufikisha matatizo yao katika mamlaka husika na sio kujichukulia hatua za kuhamishia hasira zao kwa watoto na wenza wao,” ameongeza.

Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz