Mbowe apigilia msumari wa mwisho sakata la Mdee na wenzake - EDUSPORTSTZ

Latest

Mbowe apigilia msumari wa mwisho sakata la Mdee na wenzake

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) Taifa, Freeman Mbowe, amesema chama hicho hakitabadili msimamo wake wa kumfukuza Halima Mdee na wenzake 18.Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Mbowe ametoa msimamo huo jana tarehe 6 Julai 2021, katika ziara yake ya kikazi visiwani Pemba, Zanzibar.

Ikiwa zimesalia siku kadhaa kwa Baraza Kuu la Chadema, kuketi kwa ajili ya kujadili maombi ya rufaa zao, wawaliyowasilisha kupinga uamuzi wa chama hicho kuwavua uanachama. Baraza hilo linatarajiwa kuitishwa Julai 2021.

“Wanasema kwamba kile chama cha msimamo, sasa kwa sababu kuna wabunge 19 wa viti maalumu,  tubadilishe misimamo yetu ili wale kina mama wakawe wabunge, hapana.  Sio Chadema inayoongozwa na Mbowe,  nimekataa,” amesema Mbowe.


 
Mdee na wenzake 18 walifukuzwa Chadema, tarehe 27 Novemba 2021, baada ya kukubali kuapishwa kuwa Wabunge Viti Maalumu, kinyume na msimamo wa chama hicho wa kutopeleka wawakilishi bungeni, kikisusia matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Chadema kiligoma kutambua matokeo ya uchaguzi huo, kwa madai kuwa mchakato wake haukuwa huru na wa haki. Matokeo hayo yalikipa ushindi wa zaidi ya asilimia 90,  Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika chaguzi za wabunge na madiwani.

Hata hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC), kilikanusha madai hayo, ikisema ilifuata misingi ya sheria na taratibu katika kusimamia uchaguzi huo.


Mbali na Mdee, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), viongozi wengine wa baraza hilo waliofukuzwa ni, Grace Tendega (Katibu Mkuu). Hawa Mwaifunga (Makamu Mwenyekiti). Jesca Kishoa (Katibu Mkuu) na Agnesta Lambart (Katibu Mwenezi).


Wengine waliofukuzwa ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Ester Bulaya na Esther Matiko. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Nusrat Hanje.  Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo.

Cecilia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao, Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza, nao pia walifukuzwa kufuatia sakata hilo.

Akielezea zaidi msimamo wake huo wa kutowasamehe wabunge hao, Mbowe amesema, kitendo walichokifanya kilikuwa zaidi ya ubinafsi.


 
“Nimewaambia hakuna maamuzi ya haraka kwamba tutamaliza kufanya siasa ili fulani akawe mbunge, fulani akawe diwani. Tuna ndoto kubwa ya kupigania kuleta ustawi katika nchi hii,” amesema Mbowe.

Mbowe ameongeza  “hatuwezi kuipata tukiangalia maslahi ya mtu mmoja mmoja, sisi tunaangalia maslahi yetu kama familia. Tukilia tutalia wote, tukiomboleza tutaomboleza wote. Umoja ndiyo nguvu yetu kubwa kuliko kitu chochote kingine.”

Mbowe amesema, haiwezekani ndani ya Chadema wengine wanalia,  halafu wao wanakwenda kuapishwa kuwa wabunge viti maalumu.

“Silaha pekee ya chama chetu ni umoja, mshikamano na maelewano ya ndani.  yeyote miongoni mwetu akipata maumivu tulie naye. Haiwezekani wengine wanazika,  wengine tunakwenda kuapishwa,” amesema Mbowe na kuongeza:


“Haiwezekani wengine wanatibu majeraha ya risasi, wengine wanakimbia kwenda kutafuta ruzuku, hiyo sio Chadema tunayoijenga kwa misingi ya uaminifu.”
Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz